Zaidi ya watu 12,000 wamepoteza maisha na wengine 33,000 kujeruhiwa katika machafuko ya kisiasa nchini Sudan. Picha: Reuters

Na Coletta Wanjohi

Istanbul, Uturuki

Uhasama kati ya majeshi ya ulinzi na usalama ya Sudan na wanamgambo wa RSF ulioanza Aprili mwaka jana, hadi sasa unaendelea, huku nchi hiyo kutoka kaskazini mwa Afrika ikimrejesha nyumbani balozi wake nchini Kenya baada ya sakata lililomuhusia kiongozi wa kikudi hicho, Mohamed Hamdan Dagalo.

Wakati Kenya ikifafanua yaliyojiri katika mkutano uliomuhusisha Rais Ruto na Dagalo, Januari 3, bado serikali ya Sudan imetilia shaka mchakato huo.

Mgogoro huo wa kidiplomasia unakuja wakati ambapo watu zaidi ya 12,000 wamepoteza maisha yao na wengine 33,000 zaidi kujeruhiwa kwenye machafuko yanayoendelea. Kulingana na Umoja wa Mataifa, raia milioni 6.6 wamelazimika kuyahama makazi yao.

Mwaka Mchungu

Wakati 2023, idadi kubwa ya watu wa Sudan hawakujua kuwa nchi yao ingeingia kwenye wimbo la machafuko, miezi minne baadae.

Cha kushangaza zaidi, ni kuwa pande mbili zilizofanya kazi kwa ukaribu hapo awali kumuondoa Omar al-Bashir mwaka 2019, zimekuwa ndio chanzo cha machafuko hayo.

Mapigano kati ya jeshi la ulinzi na usalama linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na RSF yalianza tarehe 15, mwezi Aprili mwaka jana.

Wananchi wa Sudan wamelazimika kuhama makwao kwasababu ya vita / picha: AFP

Mapigano hayo yalififisha kabisa matumaini ya Sudan kupata serikali ya Kidemokrasia ndani ya miaka miwili, kulingana na makubaliano ya Disemba 2022, kati ya jeshi na vyama vya kisiasa.

Kuanzia hapo, majanga ya kibinadamu yameendelea kuiandama nchi hiyo ambayo ni ya tatu kwa ukubwa wa eneo, barani Afrika.

Umoja wa Mataifa umeweka bayana kuwa, nusu ya watu wa Sudan wanahitaji msaada wa haraka, kufuatia machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini humo.

Kufikia Disemba 2023, zaidi ya watu milioni 6.6 wamelazimika kuyahama makazi yao ndani na nje ya nchi. Nchi jirani za Chad, Misri na Sudan Kusini zimelazimika kubeba mzigo wa kutoa hifadhi kwa Wasudan wanaokimbia vita.

Watu milioni 6.6, wamelazimika kuyahama makazi yao ndani na nje ya nchi, kufikia Disemba mwaka jana. Kwa namna ya pekee, nchi za Chad, Misri na Sudan zimejitolea kuwahifadhi majirani zao.

Hata hivyo, wanajeshi hao waandamizi hawajaonesha jiithada yoyote katika kumaliza machafuko hayo, hali ikiendelea kuwa mbaya.

"Jeshi la Sudan na RSF wana nguvu nyingi za kijeshi na wanahisi wanaweza kutatua matatizo yao katika uwanja wa vita," Dk Edward Githua, mtaalam wa uhusiano wa kimataifa, anaiambia TRT Afrika.

Kadiri mapigano yanavyondelea, ndivyo hali ya usalama wa chakula unavyopungua, kama unavyosababishwa na kushindwa kwa mamilioni ya wakulima kujishughulisha na kilimo.

"Takriban watu milioni 17.7 kote nchini Sudan, ambao ni asilimia 37 ya idadi ya watu waliochunguzwa, wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula, vilivyoainishwa katika IPC Awamu ya 3 au zaidi (mgogoro au mbaya zaidi) kati ya Oktoba 2023 na Februari 2024," Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa. (FAO) linasema katika ripoti yake ya hivi karibuni.

"Maeneo yenye kukabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula ni yale yalioathiriwa na machafuko hayo, ambayo yanahusisha maeneo ya Greater Darfur, Greater Kordofan na Khartoum –, hususani Sudan ya kati, Bahri na Omdurman," ripoti hiyo inaeleza.

Taarifa hiyo ya Shirika la Chakula na Kilimo Duniani inasema kumekuwepo na vitendo vya uporaji katika masoko, taasisi za kifedha, viwanda na majengo ya umma kufuatia machafuko hayo.

Kuangalia tatizo kwa undani

Kwa upande wake, Umoja wa Afrika (AU) umeendelea kusisitiza umuhimu wa kutumia njia za ndani, yaani kwa kuishirikisha nchi yenyewe katika kutafuta suluhu ya migogoro yake.

Katika mkutano wake wa 41, Shirika la Maendeleo la Kiserikali la Nchi za Afrika Mashariki (IGAD), ambalo Sudan ni nchi mwanachama, kuliwekwa mkazo wa kuunganisha Afrika kwa kupitia maridhiano.

Rais wa kenya William Ruto alikutanma na mkuu wa kikundi cha RSF Mohamed Dagalo nchini kenya Januari 2024/ Picha: Wengine 

Hata pande zinazohasimiana nchini Sudan ziliihakikishia IGAD kuwa ziko tayari kuzungumza ili kupata suluhu ya migogoro yake. Kwa mfano, Jenerali al-Burhan aliahidi kuweka silaha chini na kuwa tayari kwa mazungumzo, ikiwemo kukutana ana kwa ana na mkuu wa wanamgambo wa RSF chini ya usimamizi wa IGAD.

Hata Dagalo mwenyewe hakuwa na pingamizi lolote kwa ombi hilo.

Itoshe kusema kuwa, kwa sasa, jukumu liko upande wa IGAD kuharakisha mazungumzo shirikishi yatakayoanzisha utawala wa kiraia, ikiwa ni safari muhumu kuelekea kwenye uchaguzi wa kiraia.

Hata hivyo, swali linasalia kuwa, je, ni kweli majenerali hawa wawili wako tayari kusimamia ahadi zao? Ama kwa hakika, hili bado lina ulakini.

"Kwa sasa, ni wazi kuwa watu wa Sudan wanataka utawala wa kiraia," mjumbe maalum wa zamani wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen, Jamal Benomar, anaeleza.

Kwa upande mwingine, hakuna matokeo yoyote chanya yaliyojitokeza pamoja na vikwazo vilivyowekwa. Kwa mfano, mwaka jana, serikali ya Marekani iliziwekea vikwazo baadhi ya kampuni kwa madai kwamba yanahusika na kuchochea vurugu za kisiasa nchini Sudan.

Kampuni mbili kati ya hizi, zinadaiwa kumilikiwa na Jenerali Dagalo na nduguze. Miezi mitatu baadaye, serikali hiyo hiyo ikamuwekea vikwazo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan Ali Karti, na makampuni mawili kwa tuhumu za kuhusika kuhujumu usalama na amani wa nchi hiyo.

Mwishoni mwa mwezi huo huo, Marekani ikatangaza vikwazo dhidi ya naibu kiongozi wa RSF Abdelrahim Dagalo, kwa kukiuka haki za kibinadamu. "Kutahitajika uimara na udhabiti kutoka jumuiya ya kimataifa. Hiyo ndiyo njia pekee, kwani kuwapa nafasi (pande zinazopigana), kama walivyofanya huko nyuma, hakujazaa matunda yoyote, ni wakati wa mbinu mpya," anasema Benomar.

Darfur 'yachafua' hali ya hewa

Wakati bara la Afrika linasubiria kupatikana kwa suluhu Sudan, hofu juu ya RSF kutokuachilia maeneo inayoyahodhi inazidi kutanda.

Mkuu wa jeshi la Sudan jenerali Abdel Fattah al Burhan  aliahidi mkutano wa IGAd nchini Djibouti Desemba 2023 kuwa atafanya maongezi ya amani na mpinzani wake jenerali Dagalo/Picha wengine 

Ingawa mji mkuu wa Khartoum umekuwa kama uwanja wa vita kwa pande mbili zinazohasimiana, mapigano zaidi yameripotiwa kuongezeka katika eneo la Darfur, kwa mujibu wa ACLED.

Taasisi ya Amani Africa imeonya kuwa iwapo suala la ukosefu wa usalama nchini Sudan halitopatiwa ufumbuzi wa kudumu, kutatokea athari kubwa zaidi za kiusalama katika ukanda huu.

Miongoni mwa athari hizo kulingana na taasisi hiyo, ni kuzuka kwa makundi ya kigaidi ambayo yatasaidia kuchochea na kukuza uhalifu wa kupangwa, biashara ya uuzwaji wa silaha kiholela na uvunaji haramu wa maliasili.

Kwa sasa, macho na masikio yote yapo kwa al-Burhan na Dagalo, iwapo watasimamia ahadi zao!

TRT Afrika