Serikali ya Somalia imetangaza hali ya hatari mwezi huu kutokana na janga hilo. / Picha: AA

Zaidi ya watu milioni moja wamelazika kuhama maeneo yao nchini Somalia baada ya nchi hiyo kukumbwa na mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua kubwa, rais wa Somalia amesema.

Somalia na majirani zake wa pembe ya Afrika ikiwemo Kenya na Ethiopia wanakabiliana na athari za mafuriko ya ghafla yanayotokana na mvua kubwa za El Nino.

Mafuriko hayo yanazidisha changamoto za kibinadamu katika taifa ambalo tayari limekuwa likikabiliana na hali ngumu ya ukame wa miongo minne, ambao uliwaacha mamilioni ya watu na njaa.

"Ndugu zangu, nchi yetu iko katika hali mbaya na watu wetu wameathiriwa na mafuriko kila mahali," Rais Hassan Sheikh Mohamoud alisema Jumatano jioni.

Ameongeza kuwa watu 101 wamefariki katika mafuriko hayo.

Serikali hiyo imetangaza hali ya hatari mwezi huu kutokana na janga hilo na kuonya dhidi ya kuenea kwa magonjwa.

Hali ya 'dharura'

Katika taifa jirani la Kenya, takriban watu 120 wamefariki kutokana na mafuriko makubwa na zaidi ya kaya 89,000 zimehamishwa, hayo ni kulingana na wizara ya mambo ya ndani.

Nako nchini Ethiopia, watu wafikao 57 wamefariki kufuatia mafuriko, mvua kubwa na maporomoko ya ardhi, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kukabiliana na Masuala ya Kibinadamu.

Pembe ya Afrika ni moja ya maeneo ambayo yamo hatarini zaidi dhidi ya athari za hali ya hewa, na majanga yanayotokana na hali ya hewa yanazidi kushuhudiwa mara kwa mara.

Shirika la Action Against Hunger linasema hali ya sasa ni "mbaya."

"Maeneo ambayo yalikuwa yakijitahidi kupona kutokana na athari za kiuchumi na mazingira kutokana ukame wa muda mrefu sasa yameelemewa mara dufu na mafuriko," Shirika hilo lilisema.

AFP