Somalia itashikilia kiti hicho kwa miaka miwili kuanzia Januari 2025 / Picha/ Reuters

Somalia imechukua nafasi kama mwanachama asiye wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC. Hii ni baada ya kura ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Somalia itashikilia kiti hicho kwa miaka miwili kuanzia Januari 2025.

Somalia itaungana na wanachama wengine wanne - Denmark, Ugiriki, Pakistan, na Panama. Wote wamewahi kuhudumu katika Baraza hilo ikijumuisha Somalia mapema miaka ya 1970.

Wanachukua nafasi ya Msumbiji, Uswizi, Malta, Japan na Ecuador.

Mara ya mwisho Somalia ilikuwa kwenye UNSC ilikuwa 1972.

Je, uanachama usio wa kudumu una maana gani?

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, UNSC lina wanachana 15.

Baraza hilo linaundwa na nchi wajumbe 15.

Lina wanachama watano wa kudumu ambao ni China, Ufaransa, Urusi, Uingereza, na Marekani.

Nchi wanachama wasio wa kudumu huchaguliwa kwa misingi ya kikanda kwa muda wa miaka miwili na Mkutano Mkuu.

Haiwezekani kuchaguliwa tena mara tu baada ya kushikilia kiti katika Baraza la Usalama.

Urais wa Baraza la Usalama huzunguka kati ya wanachama wake kila mwezi, kufuatia mpangilio wa alfabeti wa Kiingereza wa majina ya nchi zao.

Baraza la Usalama lina jukumu la kudumisha amani na usalama wa kimataifa. Lina uwezo wa kuchunguza na kutatua mizozo, kuweka vikwazo, kuidhinisha matumizi ya nguvu, kuanzisha misheni ya kulinda amani na kutoa mapendekezo kwa nchi wanachama.

Baraza la Usalama hukutana mara kwa mara katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Linaweza kukutana wakati wowote, hasa katika kukabiliana na dharura na migogoro, na maamuzi yake ni ya lazima kwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa.

Maamuzi ya Baraza la Usalama yanahitaji kura za hakikisho za angalau wanachama tisa kati ya kumi na tano.

Hata hivyo, yeyote kati ya wanachama watano wa kudumu anaweza kutumia haki ya kura ya turufu, hivyo kuzuia maazimio muhimu.

Hii ndiyo sababu, utendakazi na ufanisi wa baraza wakati mwingine hutiliwa shaka.

TRT Afrika