Na Hinda Abdi Mohamoud
Wakati mizunguko inayoonekana kutokuwa na mwisho ya ukame, mafuriko na migogoro inaendelea kuwakumba wakazi wa Somalia, idadi inayoongezeka ya watu wanakimbilia viunga vya maeneo ya mijini, hasa mji mkuu Mogadishu.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa, duniani kote, watu wengi zaidi wataishi miji mikubwa kuliko vijijini ifikapo mwaka 2026.
Mogadishu inasemekana kuwa jiji la pili duniani linalokuwa kwa kasi, hasa kutokana na wimbi kubwa la watu waliokimbia makazi yao, asilimia 79 kati yao ni wanawake na watoto.
Kulingana na ripoti ya shirika lisilo la kiserikali la Refugees International, wengi wa mamilioni ya watu wanaokimbia kutoka vijijini kwenda mijini nchini Somalia hawaendi kuishi majumbani.
Wengine wameishi katika kambi za muda kwa zaidi ya miongo mitatu.
Wengi wa wakimbizi wa ndani milioni 4.3 (IDPs) nchini wanapaswa kutafuta njia mpya za kujikimu. Wengi wameishi kama wakulima na wafugaji. Hawana ujuzi wa kufanya kazi mjini. Kwa sababu hii, wanapaswa kuanza tena upya.
Fatima Mohamed Iise mwenye umri wa miaka thelathini na moja aliwasili katika kambi ya IDP ya Asal mnamo Juni 2023 na watoto wake saba. Kambi hiyo ni nyumbani kwa takriban familia 800 na ni mojawapo ya makazi mapya zaidi kutokea nje kidogo ya Mogadishu.
Alikimbia kutoka wilaya ya Qoryoley kusini mwa eneo la Lower Shabelle ya Somalia baada ya ukame kuua mifugo yake yote. Mumewe alibaki nyuma ili kulinda nyumba yao na mali nyingine chache zilizobaki.
Kazi katika migahawa
“Tulikuwa na maisha mazuri sana tukiwa wafugaji. Tulikuwa na ng'ombe wapatao 40," anasema.
"Sasa hatuna, kwa hivyo sikuwa na budi ila kuja Mogadishu na watoto wangu."
Hakukuwa na usaidizi wa kibinadamu uliopatikana kwa Lise na familia yake alipowasili katika kambi ya Asal.
Aliingiwa na hofu kwani hakujua jinsi ya kujilisha mwenyewe wala watoto wake.
Wanawake wengine waliofika kambini kabla yake walimsihi aende katika vitongoji vya jirani na kutafuta kazi.
“Mimi na binti yangu mwenye umri wa miaka tisa hutoka mapema kila asubuhi ili kutafuta kazi,” asema.
"Kazi pekee tunazoweza kupata ni kazi ya kufua nguo na kusafisha maeneo ya ujenzi ambayo hulipa kati ya $1 na $1.50 kwa siku. Hii haitoshi kulipia mahitaji ya kimsingi lakini ni bora kuliko kutofanya chochote.
"Tuna ujuzi wa mashambani pekee na hakuna anayehitaji ujuzi huu mjini."
Kambi za IDP nje kidogo ya Mogadishu zinasimamiwa na wasimamizi wa makazi yasiyo rasmi, wenyeji wanaojulikana kama ‘‘walinda lango’’, ambao hutumika kama wasuluhishi kati ya wakazi wa kambi hiyo na watendaji wa nje.
Wakaazi wa kambi ya Asal hawana kazi za kawaida. Kama Lise na binti yake, wao huenda nje kila asubuhi kutafuta kibarua. Njia za kawaida za kazi ambazo wanawake hupata ni kusafisha nyumba za watu, kufua nguo zao na kuosha vyombo kwenye mikahawa.
Watoto huanza kufanya kazi kutoka umri wa miaka minne au mitano. Wasichana huosha vyombo, wavulana hupiga viatu kiwi au kufanya kazi katika mikahawa.
Pesa wanazopata, ni kati ya $1 na $2 kwa siku wanapopata kazi, huku wakibaki kwenye mzunguko wa umaskini.
Hali ngumu
“Natumia mapato yangu kununua mchele, maharagwe au unga wa mahindi. Tunakula mara moja kwa siku wakati wa chakula cha mchana,” asema Lise.
Wakati uliobaki tunakunywa chai. Mimi na watoto wangu huenda kulala tukiwa na njaa."
Kama wanawake wengine waliokimbia makazi yao, Lise anakabiliwa na changamoto ya ziada ya unyanyasaji kutoka kwa wanaume, hasa wanachama wa vikosi vya usalama, wasimamizi wa kambi na wengine katika nyadhifa za mamlaka.
Makazi katika kambi yametengenezwa kwa vijiti na plastiki na wakimbizi wa ndani mara nyingi hawana nguo nzuri. Wanaume mara nyingi huwaendea wanawake na wasichana kwa vitendo viovu ili kupata chakula au ajira.
“Wanaume huja kwangu wakitaka kunisaidia kutafuta kazi au kupata chakula,” asema Lise.
"Kisha wanasema wanataka kitu kama malipo."
Hawa mwenye umri wa miaka sabini (sio jina lake halisi) na mjukuu wake wa kike mwenye umri wa miaka mitatu wamekuwa wakiishi katika kambi ya Asal kwa miezi saba.
Alipofika mara ya kwanza, alikuwa mmoja wa watu wachache waliobahatika kupokea msaada wa kibinadamu.
Lakini msaada ulisitishwa mwezi Mei baada ya kukataa ombi la ‘’ lisilo la maadili’’ kutoka kwa mmoja wa wanaume wanaosimamia kambi hiyo na kudhibiti usambazaji wa misaada.
"Hali ya maisha yangu sasa, hayawezi kuazwa na mtu yeyote. Ni vigumu kuamini sababu ya kutopokea tena msaada wa chakula lakini huo ndio ukweli.”
Maisha ya kuhamahama yaliisha
"Msimamizi wa kambi hiyo aliniomba nijihusishe na tabia fulani mbaya ikiwa nilitaka chakula," anasema Hawa.
“Nilishtuka na kwa hasira nikamkatalia. Tangu wakati huo sijapokea hata punje moja ya chakula.”
Hawa anasema kumekuwa na visa vingi sawa na vyake. “Inahuzunisha sana,” anaongeza.
"Hali ni bora kwa wakimbizi wa ndani ambao wanafanya kazi katika nyumba za watu kwa sababu ni wanawake ambao wanabaki nyumbani wakati wanaume wanatoka kwenda kazini," Hawa anasema.
"Waajiri ambao ni wema kwetu ni wanawake wazee. Wakati fulani wanatupa pesa za ziada.”
Kwa kuwa sasa hapokei tena msaada, Hawa anaondoka kambini kila asubuhi kutafuta kazi ya kusafisha katika maeneo ya ujenzi na mikahawa.
Wakati mwingine yeye hufua nguo kwa familia katika vitongoji vya karibu. Kawaida humchukua mjukuu wake kufanya kazi naye. Wakati mwingine anamwacha chini ya uangalizi wa wanawake wengine huko Asal.
Mmoja wa wanawake waliokata tamaa katika kambi hiyo ni S’iido Hassan Moalim. Alilazimika kuachana na maisha yake ya kuhamahama katika wilaya ya Kuntuwaarey huko Lower Shabelle baada ya ukame kukausha ardhi na kuharibu mifugo yake yote.
Moalim hajaolewa na hajawahi kupata watoto. Ana umri wa miaka sitini na sita na mlemavu wa macho.
Kufua nguo
"Ninaishi hapa peke yangu," anasema Moalim. “Naamini mimi ndiye mtu maskini zaidi katika kambi hii. Sioni, siwezi kufanya kazi na sijapokea kadi za vocha za msaada wa chakula."
Majirani wa Moalim wakati mwingine hushiriki naye kile walicho nacho lakini mara nyingi yeye hana chochote. "Wanyonge hawana haki," anasema.
Lisho Mukhtar Adam aliwasili katika kambi ya Asal mwishoni mwa Juni 2023 baada ya mapigano katika wilaya ya Kuntuwaarey kumlazimisha kutoroka nyumbani kwake na wanawe watatu wachanga.
Alianza kufanya kazi ya kusafisha na kuosha nguo karibu mara moja na anaweza kuwanunulia watoto wake chakula kwa mapato yake.
"Ninafua nguo na kusafisha nyumba za watu ambao wana hali nzuri kuliko mimi," anasema.
“Mimi hupata kati ya $1 na $2 kwa siku. Ninafanya kazi kwa saa nyingi ili kusimamia maisha ya familia yangu kadiri niwezavyo.”
Adam anaelezea jinsi wakimbizi wa ndani wanaofanya kazi katika nyumba za watu hupigwa mara kwa mara na waajiri wao ambao wakati mwingine huwashutumu kwa kuiba mali zao.
"Mwisho wa siku, watu wengine wanasema hawana pesa za kutulipa na kwamba tunapaswa kurudi siku inayofuata kuzichukua," anasema.
“Wengine hawatulipi kabisa. Hawatuheshimu. Waajiri wengi wanatudharau lakini baadhi ya watu waliosoma zaidi wanatuchukulia kuwa bora zaidi.”
Anasema kumekuwa na msaada mdogo. Polisi wanaelekea kuwa na shughuli nyingi kukabiliana na vitisho vya usalama vya Mogadishu vinavyoletwa na magaidi wa Al Shabab.
“Hakuna mtu anayetusikiliza,” asema Adam. "Kitu pekee cha kufanya ni kuviambia vyombo vya habari kuhusu masaibu yetu na kutumaini kwamba mtu aliye na uwezo na rasilimali kufanya hivyo atatusaidia," anaomba kupata watu wa kuwapa msaada.
"Watu wengi hunyamaza kuhusu hilo kwa sababu wanajua kwamba wakilalamika watafukuzwa kambini."
'Nataka kuanzisha biashara'
Watu wanaoishi katika kambi moja ya zamani zaidi ya wakimbizi wa ndani, Mogadishu, inayojulikana kama Allah dhowr, wanapata matatizo sawa na wale wa Asal.
Rahma Mohamed aliwasili huko na mumewe na watoto wanne mnamo Januari 2022 baada ya ukame kuua mifugo ya familia hiyo katika wilaya ya Kuntuwaarey kusini mwa Somalia.
Kila siku Mohamed na mumewe huamka alfajiri na kutembea hadi kwenye vitongoji vya jirani kutafuta kazi. Wanawaacha watoto wao kwa wakazi wenzao wa kambi hiyo.
"Mara nyingi watu ninaowafanyia kazi wananilipa kidogo kuliko tulichokubaliana," anasema.
"Tunaweza kukubaliana $5 lakini mwisho wa siku watanilipa $3 pekee."
Licha ya changamoto zilizopo mjini Mogadishu, Mohamed hana nia ya kuondoka.
"Licha ya kutazamwa na watu kama mkimbizi, nataka kuanzisha biashara yangu ndogo hapa ili kusaidia familia yangu."
Asmo Abdi Farah Ahmed mwenye umri wa miaka 15 alienda madrasa ya kufunzwa Korani katika wilaya ya Mushaan kabla ya ukame kumlazimisha kukimbilia Mogadishu mwaka 2023.
Sasa anafanya kazi pamoja na mama yake kama mfanyakazi wa nyumbani na muoshaji nguo.
"Watoto katika vitongoji vinavyozunguka kambi yetu huenda shuleni na kucheza pamoja," anasema. “Wakati fulani wananidhihaki kwa kutokwenda shule. Wanasema mimi ni ‘mtoto wa kijijini’ tu”.
Hata wale ambao wameishi Mogadishu kwa miaka mingi wanadharauliwa na kuonekana kama wakazi wa muda.
Suluhisho liko njiani "Watu hapa bado wananichukulia kama mtu aliyehamishwa, mkimbizi, ingawa nimeishi hapa kwa miaka 16," anasema Mukhtar Abdalla Abdow mwenye umri wa miaka 60.
Alikimbia eneo la nyumbani kwake la Janaale zaidi ya miaka 30 iliyopita, kwanza hadi katikati mwa jiji la Galkayo, kisha Mogadishu.
"Ninajiona kuwa mkazi wa eneo hilo," anasema.
"Wakazi ndani wa muda mrefu wanafanana kwa karibu zaidi na maskini wa mijini na wana mahitaji tofauti kuliko wanaowasili,'' Shirika la Refugees International inasema.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa Mogadishu, kama Juweeriya Mohamed Ibrahim, wana mtazamo wa kukaribisha wakimbizi wa ndani.
"Ninawaona kama watu wa kawaida waliokuja hapa kwa sababu maisha yao yalitishiwa na mafuriko, ukame na migogoro," anasema.
"Kwangu mimi, kama wameishi Mogadishu kwa zaidi ya miaka mitano, ninawachukulia kuwa wakazi kama mimi."
“Wengine mara nyingi wanasema ni raia wa daraja la pili. Ninaamini kabisa hawako hivyo.”
Kama sehemu ya ufumbuzi wa matatizo ambayo watu waliokimbia makazi wanakabiliana nayo, serikali ya Somalia ilitangaza mpango wa kuwapa makazi wakimbizi wa ndani na kuboresha hali zao za maisha.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo Hamza Abdi Barre alizindua Mpango Kazi wa Njia za Kitaifa za Suluhu mnamo Septemba 4 huko Mogadishu, na kuongeza matumaini juu ya hali mbaya ya wakazi wa ndani.
Mpango huo wa miaka mitano unatarajiwa kuanza mwaka huu hadi 2029.
"Wasomali milioni moja kurejea katika maisha ya kawaida itakuwa hatua muhimu ya kutafuta suluhu la kudumu kwa waliokimbia makazi yao ili waweze kuwa sehemu ya jamii kwa maendeleo ya nchi," waziri mkuu alisema.
Mwandishi, Hinda Abdi Mohamoud, ni Mhariri Mkuu wa Bilan, chombo cha habari cha kwanza cha wanahabari wanawake nchini Somalia lenye makao yake makuu mjini Mogadishu.