Na Edward Qorro
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Somalia, mwanachama mpya ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) itachagua Jaji, Waziri na wabunge watakaoiwakilisha nchi hiyo ndani ya Jumuiya hiyo.
Haya ni sehemu ya matakwa ya kisheria kwa nchi hiyo ambayo hivi karibuni imejiunga na Jumuiya hiyo yenye nchi nane.
Tayari, Somalia imeshawasilisha nyenzo za kuridhia uanzishwaji wa Jumuiya hiyo, kwa mujibu wa kifungu namba 153 cha itifaki ya uanzishwaji wa Jumuiya hiyo.
Hata hivyo, nchi hiyo pia itawajibika kuchagua Waziri anayehusika na masuala ya Afrika Mashariki, Jaji na wabunge, kuzingatia kifungu namba 8(3) cha itifaki hiyo, kulingana na Dk Anthony Luyirika Kafumbe, ambaye pia ni mwanasheria wa EAC.
"Huu ni mwanzo tu wa Somalia kuanza kutekeleza majukumu yake mengi kama mwanachama mpya wa Jumuiya yetu," anasema Dk Kafumbe, wakati wa hafla ya kuwasilisha nyenzo hizo.
Nchi hiyo, ambayo iliidhinishwa na mkutano wa kawaida wa 23 wa wakuu wa nchi za EAC uliofanyika Arusha, Tanzania Novemba 2023, itachagua wajumbe 9 wa kuiwakilisha katika Bunge la Afrika Mashariki(EALA) na Jaji mmoja ndani ya Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki(EACJ).
Moja ya majukumu yanayoikabili Somalia baada ya kujiunga na Jumuiya hiyo yenye watu takribani milioni 350 ni michango ya mara kwa mara, ambayo bado inaonekana kusuasua kati ya nchi wanachama.
"Leo ni siku kubwa sana kwetu, kama Somalia, tunaahidi kutekeleza majukumu yetu yote kama nchi wanachama," anasema Jibril Abdirashid Haj Abdi.
Pamoja na majukumu mengine, Somalia itakuwa inakabiliwa na kazi ya kuoanisha itifaki ya EAC na sheria za ndani ya nchi hiyo, kama moja ya masharti kwa nchi wanachama.