Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alisema nchi yake "itajilinda" ikiwa Ethiopia itaendelea na makubaliano ya kuanzisha kituo cha jeshi la wanamaji katika eneo lililojitenga la Somaliland na ikiendelea kutambua eneo hilo kama taifa huru.
"Ikiwa Ethiopia itasisitiza, Somalia itapinga na itakataa," Mohamud aliiambia Reuters siku ya Jumanne katika mahojiano katika ikulu ya rais iliyo na ulinzi mkali mjini Mogadishu.
"Kama watakuja nchini, Somalia itafanya kila iwezalo kujilinda."
Ethiopia isiyokuwa na bandari ilikubali mkataba wa maelewano Januari 1 kukodisha kilomita 20 (maili 12) za mwambao wa Somaliland - eneo ambalo Somalia inasema inamiliki, ingawa eneo la kaskazini limekuwa likisisitiza kujitawala tangu 1991.
Ethiopia ilisema inataka kuanzisha kituo cha jeshi la wanamaji huko na kutoa uwezekano wa kuitambua Somaliland badala yake - na hivyo kusababisha jibu la dharau kutoka kwa Somalia na inahofia kuwa mpango huo unaweza kuyumbisha zaidi Pembe ya Afrika.
Rais Mohamud alisema atakubali tu kujadili suala hilo na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed wakati serikali ya Addis Ababa itakapobatilisha nia yake ya "kuchukua sehemu ya nchi yetu".
Rais huyo wa Somalia hakuelezea kwa undani zaidi kuhusu hatua ambayo Somalia inaweza kuchukua.
Pembe ya Afrika imekumbwa na migogoro ya mara kwa mara, iliyochochea migogoro ya kibinadamu katika maeneo yanayokumbwa na ukame. Nchi jirani za Ethiopia na Somalia zilipigana juu ya eneo hilo mnamo 1977-1978 na 1982.
Japo Serikali ya Ethiopia haijazungumzia tangazo hili, Waziri mkuu Abiy alisema hapo awali Ethiopia haina mpango wa kuanzisha mzozo na Somalia na inajaribu tu kushughulikia hitaji lake la ufikiaji wa bahari.
Tishio la kijeshi
Rais Mohamud alisema hazingatii kuwatimua karibu wanajeshi 3,000 wa Ethiopia walioko Somalia kama sehemu ya ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika unaopambana na wanamgambo wa al Shabaab, wanaohusishwa na al Qaeda.
Wachambuzi na wanadiplomasia wanahofia kuondoka kwa wanajeshi wa Ethiopia kutazidi kuyumbisha Somalia, ambapo mashambulizi ya al Shabaab yameua maelfu ya raia na wanajeshi tangu mwaka 2006.
Somalia na nchi kadhaa za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani, ambayo mara kwa mara hufanya mashambulizi dhidi ya wanamgambo nchini Somalia, zimesema makubaliano ya bandari ya Ethiopia yameongeza juhudi za kuwasajili al Shabaab.