Zaidi ya watu 70 walifariki katika maporomoko ya ardhi yaliyotokea wilaya ya Katesh Mkoani Manyara Tanzania / Picha : TRT Afrika 

Ronald Sonyo

TRT Afrika, Dodoma, Tanzania

Mwishoni mwa mwaka jana sio kumbukumbu nzuri kwa watu wa vitongoji vya karibu vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay na Sebasi, Wilayani hana’g Mkoani Manyara kaskazini mwa nchi ya Tanzania. Wengi hawajui jinsi watasahau kilichotokea.

Hii ilikuwa alfajiri ya huzuni, ukiwa na simanzi mtawalia baada ya mafuriko ya mvua yaliosababishwa na mmeguko wa miamba dhoofu iliyosomba mawe, magogo ya miti na tope kutoka katika mlima hanan,g kusababisha vifo vya watu, Mifugo, kuharibu miundombinu ya barabara, Makazi pamoja na biashara.

Kuna mwendo wa saa tano kwa usafiri wa barabara kuingia mjini mdogo wa katesh Wilayani Hanan’g, Mkoani Manyara na umbali wa km 323. 4 kutokea makao makuu ya nchi Dodoma, huku upande wa Mkoa wa Arusha kuingia mjini humo una km 236.8 tofauti na umbali wa kutokea Singida wenye km 95.

Ni mji uliojulikana kwa shughuli za biashara na njia kuu ya kuingia Mkoa wa Arusha na kilimanjaro kabla ya njia nyingine ya kuingia mikoa hiyo kuazishwa mwaka 2016, lakini baadhi kwa hivi sasa wanapajua Katesh, kupasikia ama hata kufika na wengine wakitamani kufika na kushuhudia atahari zilizotokea .

Hata hivyo, hivi sasa ukifika mjini humo taswira ni tofauti kwani sehemu ambapo hakukuwa na bonde sasa kuna mabonde, mikondo ya maji, na vifusi na kule ambapo kulikuwa na masoko, makazi, na shughuli nyengine za kijamii kwa sasa huenda usikute na kama ukikuta basi sio kwa uhalisia wa mwazo.

Zilipokuwa Nyumba imesalia mahame, utaona pia samani ya vitu vya ndani kama meza, Vitanda na vyombo mbalimbali zisizofaa tena kwa matumizi kutokana na kiwango cha uharibifu.

Ingawa ni uharibifu huu umemgusa kila mtu kwa sehemu yake, lakini huenda walioathirika zaidi ni wafanyabiashara wa bidhaa katika soko kuu la katesh, huku takriban wafanyabiashara zaidi ya 200 wamehamishwa katika soko la muda maarufu soko mjinga.

Hatua hii ni katika jitihada ya Serikali ya nchi hiyo kuwafanya waathirika kuendelea na maisha yao kawaida. Unapofika sokoni hapo utaona vibanda vingi watu wakiendelea na pilikapika, lakini ni wazi kuna hali ya upweke mjini.

Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza vyombo vya serikali kusimamia shughuli zote za uokoaji, matibabu na mazishi kwa waathiriwa wa maporomoko hayo ya ardhi ya Mkoa wa Manyara / Picha : TRt Afrika 

Siwema Khamiss anaendelea kukata mboga tayari kwa ajili ya kumuuzia mteja aliyesimama kwa pembeni. Aliiambia TRT kwamba hali ya soko jipya sio shwari, kwani hakuna biashara na hawana mitaji walioupata ili kufidia sehemu ya athari zilizowapata ili kuendelea na maisha ya kawaida ya kujikimu.

Hata hivyo, amesema asingetamani kukumbuka yaliotokea nyuma (mafuriko) na hana shauku tena ya kurudi katika soko lile hata kwa adhabu yeyote, lakini aliwalaumu baadhi ya watendaji wa ngazi za chini kwa kutowajibika sawasawa na maagizo ya Serikali kuu ya kugawa misaada sawa kwa watu wote.

“Tangu tumetoka kwenye lile soko letu kule na kuletwa hapa kwa kweli biashara ni ngumu sana, wateja wanapata shida hasa kipindi cha mvua hakuna pa kukinga mvua wala jua, lakini sintorudi kule hata kwa fimbo” Alisema.

“Ukipata hela ya kula unashukuru mungu, huwezi kuwa na akiba kwa ajili ya watoto na tunaomba Serikali itutazame kwani hatuna makazi wala mitaji ya kuendesha biashara zetu” Aliongeza.

Serikali imesema inawajengea waathiriwa nyumba za muda, shule na masoko ya muda kuwezesha kuendelea na shughuli zao kwa sasa / Picha : TRt Afrika 

Wengi wanakiri mji umepwya na taswira kubadilika. “Hili janga limewahamisha watu wengi sana kutoka walikozoea hadi maeneo mengine mfano Jorodom kaya zilizoondoka ni nyingi na unakuta familia moja imebakiwa na mtu mmoja wengine wamefariki” Alisema Regnad Soka ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo na pia ni mwenyekiti wa wafanyabiashara hao.

“Sisi wauza nyanya tumesahaulika sana, na watu wafanye haki wamuogope Mungu, misaada inaletwa lakini haitufikii sisi, na hii misaada mtu katoa sadaka yake hujua kaisemea vipi lakini haitufikii sisi na Rais anajua sisi tunapata misaada lakini sio kweli” Alisema Husna Zuberi Mfanyabiashara wa mboga.

“Bado hatuna mitaji na tunaomba Serikali ifanye bidi turudi Sokoni, Hatuna mitaji na nimeshikwa mkono na ndugu zangu tu kwani mizigo yote iliondoka, Serikali itushike Mkono” Aliongeza Husna

Hata hivyo, misaada imeanza kuwafikia wafanyabiashara hao. Mkuu wa Mkoa huo Queen Sendiga amesema Serikali ipo tayari kutatua vikwazo vinazowakabili waathirika wakiwemo wafanyabiashara. Alizungumza na wafanyabaishara hao akiwa eneo la tukio baada tu ya kumaliza kugawa vyakula.

“Leteni malalamiko yetu na tutazishughulikia ili maisha yarudi kawaida” Alisema Sendiga.

Sasa ni mwezi mmoja tangu maafa hayo kutokea na huku mvua nazo zikiendelea kusababisha hasara Serikali ya nchi hiyo nayo licha ya kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika pia imetenga eneo maalum la kujenga makazi zaidi ya 100 pamoja na kuanzishwa kwa shule ya muda katika kitongoji la Hararack kilichojitenga baada ya mafuriko ikilenga kutoa masomo kwa wanafunzi wa arasa la 1,2 na 3 .

TRT Afrika