Huu ulikuwa ni ushindi wa pili kwa Lemma mweye umri wa miaka 32 na ambaye sasa amekimbia mbio 24 za marathon katika kipindi cha miaka kumi./ Picha : X - Adidas Running

Na Lynne Wachira

TRT Afrika, Nairobi, Kenya

Vyombo vya habari na wachanganuzi wengi wa riadha hakumuangazia wala kumpigia upato Sisay Lemma kati ya wanariadha waliotarajiwa kuandikisha matokeo ya kufana katika mashindano ya mbio za Valencia ambayo yamekamilika mapema leo huku Lema akiandikisha ushindi katika upande wa wanaume.

Mbio zilianza wanariadha wakiwa pamoja huku macho yote yakiwa kwa Joshua Cheptegei wa Uganda na Kenenisa Bekele wa Ethiopia, na kama ilivyo kawaida katika mbio zilizo na ushindani mkali, kikundi cha zaidi ya wanariadha kumi kilisalia kwa pamoja katika takriban kilomita ishirini za kwanza.

Wanariadha katika kundi la uongozi waligawanyika punde tu walipopita kilomita 21 kwa kutumia muda wa saa moja pekee – Sisay Lemma alisalia katika uongozi ishara tosha kuwa aliamini uwezo wake kutwaa ushindi.

Ni katika kilomita chache pekee ambapo mkenya Kibiwott Kandie alichukua uongozi huku Lemma na Gerald Geay wa Tanzania wakifuata kwa karibu kabla ya Lemma kunyakua uongozi tena baada ya kilomita thelathini na tano na akaongeza kasi pasiwe na wa kumfuata wala kumpiku.

Lemma hatimaye alinyakua ushindi na kuvunja rekodi ya mbio za Valencia kwa kuandikisha muda wa 2:01:48. Rekodi ya hapo awali ya 2:01:53 iliandikishswa na Kevin Kiptum.

Huu ulikuwa ni ushindi wa pili kwa Lemma mweye umri wa miaka 32 na ambaye sasa amekimbia mbio 24 za marathon katika kipindi cha miaka kumi.

Alexander Mutiso ambaye alimaliza katika nafasi ya tatu mwaka uliopita alimaliza katika nafasi ya pili huku Dawit Wolde wa Ethiopia akikamilizia orodha ya tatu bora.

Hakuandikisha ushindi lakini Kenenisa Bekele alipata mafanikio

Mshikiliaji wa zamani wa rekodi ya dunia ya mita elfu tano na mita elfu kumi Kenenisa Bekele alimaliza katika nafasi ya nne na kuandikisha rekodi mpya (2:04:19) ya dunia ya Masters yaani kwa wanariadha walio na umri wa zaidi ya miaka 40.

Wakati huo huo ndoto yake ya kuandikisha muda wa kufuzu kushiriki michezo ya olimpiki mwaka ujao mjini Paris ilitimia, kwa sasa atasubiri shirikisho la riadha la Ethiopia kutaja kikosi chake cha taifa.

Bekele alishiriki mashindano yake ya mwisho mapema mwaka huu katika mbio za mji mkuu wa Uingereza, London.

Worknesh Degafa anyakua ushindi baada ya kurejea kutoka mapumziko ya kujifungua /Picha : X-  Adidasrunning 

Katika mbio za upande wa wanawake Worknesh Degefa alitwaa ushindi katika mashindano yake ya kwanza tangu kurejea baada ya kuchukua muda wa mapumziko kujifungua akitumia muda wa 2:15:51.

Degefa alikabiliana na ushindi mkali kutoka kwa Almaz Ayana huku muethiopia mwingine Hiwot Gebrekidan akihakikishia Ethiopia nafasi tatu bora.

Jedwali ya matokeo

Wanawake

1. Worknesh Degefa (ETH) - 2:15:51

2. Alaz Ayana - 2:16:22

3. Hiwot Gebrekidan - 2:17:59

4. Celestine Chepchirchir - 2:20:46

5. Majida Maayouf - 2:21:27

6. Sultan Haydar - 2:21:27

7. Desi Mokonin - 2:21:29

8. Genevieve Gregson - 2:23:08

9. Sofiia Yaremchuk - 2:23:16

10. Isobel Batt-Doyle - 2:23:27

Wanaume

1.Sisay Lemma (ETH) - 2:01:48 CR

2. Alexander Mutiso - 2:03:11

3. Dawit Wolde - 2:03:48

4. Kenenisa Bekele - 2:04:19

5. Gabriel Geay - 2:04:33

6. Kibiwott Kandie - 2:04:48

7. Chalu Deso - 2:05:14

8. Mohamed Esa Huseydin - 2:05:40

9. Mehdi Frere 2:05:43

10. Gashau Ayale - 2:05:46

TRT Afrika