Na Nuri Aden
Kulingana na takwimu za hivi karibuni, idadi ya Twiga ulimwenguni imetajwa kupungua hadi 117, 000 huku ongezeko la visa vya ujangili ikilaumiwa kusababisha upungufu wa idadi ya wanyama hao.
Mauaji ya wanyama hao pia imeathiri mapato ya kitalii kwa mataifa mengi Afrika huku twiga wakilengwa kwa biashara iliyonoga ya nyama yao. Hilo limesababisha wanyama hao kuwekwa chini ya ulinzi wa vikundi vya kukabiliana na ujangili.
Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (UCN) umejumuisha speshi za Twiga za Nubian na Kordofan hadi kiwango cha wanyama walioko hatarini na kufikia sasa zimesalia takriban twiga 4,650.
Fahamu zaidi kuhusu Twiga
Barani Afrika, Twiga wa Kusini ndio aina ya twiga walio wengi zaidi huku idadi yao ikiwa ni takribani twiga 49,867, ambapo twiga 29,675 wakipatana nchini Afrika Kusini na twiga 20,192 ni wa Angola.
Hata hivyo, Afrika Mashariki ni ngome ya twiga Afrika huku zaidi ya asilimia 50 ya twiga kwa jumla wakipatikana eneo hilo.
Nchi ya Kenya pia inaelezwa kuwa taifa lenye aina tatu ya Twiga; Twiga wa Reticulated hupatikana kaskazini na mashariki mwa Kenya; Twiga wa Kimasai wanaoishi savanna na misitu ya kusini mwa Kenya; na twiga wa Nubia (zamani twiga wa Rothschild). Kwa jumla, Kenya ina twiga 34, 530.
Takwimu zaidi zinaonyesha kuwa kwa kila Ndovu wanne, kuna Twiga moja. Yaani, idadi ya ndovu ni mara nne ya Twiga.
Je, ni sifa zipi zinamfanya Twiga kuwa kiumbe cha ajabu?
Katika kila kipindi cha saa 24, Twiga huhitaji tu kulala kwa dakika 5 hadi 30. Mara nyingi wanafanikisha hilo kwa usingizi wa haraka ambao unaweza kudumu dakika moja au mbili kwa wakati mmoja.
Cha kustajaabisha ni kuwa, madoa ya twiga mmoja ni tofauti na ya twiga mwingine kama alama za vidole vya binadamu vilivyo. Hakuna twiga wawili walio na muundo sawa wa madoadoa. Kila twiga anaweza kuwa na hadi madoa 450.
Ingawa ni mnyama mwenye kimo kirefu, Twiga hutaabika kufika chini wakati wa kunywa maji kutokana na ufupi wa shingo lake. Hali hiyo humlazimu kutandaza miguu yake ya mbele kwa shida au kupiga magoti ili kufikia chini kwa ajili ya kunywa maji.
Kwa jumla, Twiga huishi maisha ya hadi miaka 25 wakiwa porini na hadi miaka 28 wakiwa kifungoni. Hata hivyo, twiga wengi hawajaliwi kuishi hadi muda huo kutokana na vitisho kama vile ujangili na kupoteza makazi kutokana na changamoto zinazotokana na tabia nchi, na masuala mengine.
Kipindi cha ujauzito kwa twiga ni takriban miezi 15. Twiga jike huzaa ndama mmoja, na atamtunza ndama huyo kwa hadi miezi 22 au takriban mwaka mmoja na miezi 10.