Idadi ya sokwe duniani kote imepungua kwa miaka mingi, huku sokwe wa magharibi wakikadiriwa kupungua kwa 85%, hii ikiwa ni kupungua kwa kiasi kikubwa tangu miaka ya 1980.
Jamii ndogo zote nne za sokwe zinakabiliwa na kutoweka leo, kulingana na Jumuiya ya Uhifadhi Ulimwenguni. Nyani wana jukumu muhimu katika kudumisha utofauti wa misitu.
Wanyama hao wanawindwa kwa ajili ya nyama ya porini au kulazimishwa kutoka katika makazi yao kwa ukataji miti kibiashara na kilimo, kulingana na Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN).
Ingawa sokwe hao wanatishiwa zaidi na usafirishaji kibiashara kwenye mbuga za wanyama na maabara za utafiti, wahifadhi wanajitahidi kulinda idadi ya sokwe inayopungua, ambayo kwa sasa inakadiriwa kuwa kati ya 170,000 na 300,000, kulingana na wakfu wa hifadhi ya Wanyamapori Ulimwenguni (WWF).
Mambo muhimu juu ya Sokwe
- Anaweza kuishi hadi miaka 80
- Sokwe aliyepewa jina la Little Mamma ndiye sokwe mkongwe kuishi akiwa na umri wa 76 - 82 wakati wa kifo chake 2017.
- Muda wa wastani wa kuishi kwa sokwe waliofungwa ni takriban miaka 38, lakini maisha ya sokwe porini ni ngumu zaidi kurekodi.
- Utafiti wa sokwe katika Mbuga ya Kitaifa ya Kibale nchini Uganda unakadiria kwamba sokwe wastani huishi hadi miaka 33.
- Huzaa mara moja kila baada ya miaka mitano
- Mimba nyingi za sokwe hubeba mtoto mmoja.
- Wana desturi ya kuwabeba wanao kila wakati na kuwanyonyesha, na hii husababisha uhusiano wa karibu wa kifamilia, hata wakati wa ukomavu.
- Muundo wa familia zao ni ngumu kuelewa
- Vikundi vya familia vilivyopanuliwa vinaweza kukua hadi kufikia sokwe 20 hadi 120
- Wanaishi kwa mfumo wa kuongozwa na dume la alpha. Wanaishi katika vikundi ambapo ukubwa wa uanachama na muundo hubadilika kadri muda unavyopita. Vitengo vipya vidogo mara nyingi huunda wanyama wanapoanzisha uhusiano mpya.
- Wanao uwezo wa kutumia zana za kujitengenezea ili kujilisha na kujilinda. Miamba na vijiti ni baadhi ya zana za kimsingi wanazotumia kutafuta chakula. Pia hutumia matawi ya miti kuchana migongo yao.
- Sokwe hula mchanganyiko wa vyakula ikiwemo mimea na wanyama. Wao, hata hivyo, hupendelea zaidi kula matunda. Chakula cha sokwe ni pamoja na mbegu, majani, mizizi, wadudu na asali. Wakati mwingine huwinda na kula wanyamapori wengine kama nyani au swala wadogo.
- Sokwe kawaida hutembea kwa miguu minne, lakini pia wana uwezo wa kutembea kwa miguu miwili. Wao, hata hivyo, huzunguka kwa kupanda na kubembea kutoka mti hadi mti.