Wananchi Rwanda na wageni kutoka nchi mbali mbali wameungana katika eneo chini ya Hifadhi ya Kitaifa ya Volcano huko Kinigi, Musanze, kwa ajili ya sherehe maalumu ya kuwapa sokwe majina.
Kwita Izina ni sherehe ya kuwapa sokwe waliozaliwa majina. Mwaka huu sokwe 23 waliozaliwa katika kipindi cha miezi 12 iliyopita watapewa majina.
"Kwita Izina si tukio tu, ni heshima kwa sokwe wa milimani na jumuiya zilizojitolea zinazotetea uhifadhi wao," Clare Akamanzi, afisa mkuu mtendaji wa Bodi ya Maendeleo ya Rwanda amesema.
Hii ni sherehe ya 19 nchini humo.
Serikali ya Rwanda huchagua watu maarufu nchini na kutoka nchi zingine katika kila tasnia, wakiwemo mabingwa wa uhifadhi, watu mashuhuri, viongozi, magwiji wa michezo pamoja na watu wa kawaida.
Mwaka huu Elvine Ineza mtoto wa darasa la sita katika shule nchini Rwanda amepewa fursa ya kumpa sokwe jina.
Waigizaji maarufu wa Marekani Idris Elba na Kevin Hart pia ni kati ya wale walioteuliwa kuwapa sokwe majina.
Kwa nini Rwanda inawapa Sokwe majina?
Rwanda ilianza kuwapa majina sokwe wa milimani mwaka 2005, katika kile ambacho kimekuwa sasa sherehe ya ulimwengu ya asili.
Jumla ya sokwe watoto 374 wamepewa majina tangu Kwita Izina ya kwanza kufanyika.
Bodi ya Maendeleo ya Rwanda inasema kwa kuwapa majina wanyama hawa wakubwa, inawapa thamani wanayostahili.
" Sherehe, kwanza kabisa, ni fursa ya kuwashukuru wanajamii wanaoishi karibu na makazi ya sokwe, Hifadhi ya Kitaifa ya Volcano, washirika wa utafiti, madaktari wa mifugo na wahifadhi waliojitolea, walinzi na wafuatiliaji wanaolinda sokwe kila siku," bodi hiyo imeelezea katika tovuti yake.