Na Kudra Maliro
Huku idadi ya vifaru barani Afrika ikiendelea kupungua, Mbuga ya Kitaifa ya Garamba katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imepata ongezeko.
Vifaru kumi na sita weupe wametolewa katika hifadhi ya wanyama ya kibinafsi huko Kwa-Zulu Afrika Kusini - na kuongeza idadi ya wanyamapori katika mbuga ya Garamba. Vifaru ni miongoni mwa wanyama pori wanaokabiliwa na vitisho kutoka kwa wawindaji haramu.
Faru mweupe wa mwisho katika Mbuga ya Kitaifa ya Garamba, iliyoko kaskazini-mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, aliwindwa mwaka 2006 - na kuacha mbuga hiyo maarufu ikiwa haina hata mmoja. Lakini matumaini yanakuzwa sasa kwa kutoa njia mbadala.
Furaha na matumaini
"Kurejea kwa faru weupe katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kunaonyesha dhamira ya nchi yetu katika kuhifadhi viumbe hai," alisema Yves Milan Ngangay, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Congolais pour la conservation de la nature (ICCN) au Taasisi ya Kongo ya Uhifadhi wa Mazingira.
Zoezi hilo lilifanywa na ICCN, shirika lisilo la kiserikali la African Parks na kampuni ya uchimbaji madini ya Canada, Barrick Gold, ambayo ilifadhili harakati za faru hao.
Video iliyotayarishwa na African Parks inaonyesha walinzi wa mazingira wakiwaachia faru weupe katika Hifadhi ya Kitaifa ya Garamba saa chache baada ya kuwasili kutoka Afrika Kusini.
“Tunafuraha kuona viumbe hawa kwa mara nyingine tena katika mbuga yetu ya Garamba, na tunatumai kuwa watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia watakuja tena kutembelea eneo letu,” anasema Maguy Nabintu, mfanyakazi wa kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick Gold Corporation, ambaye. alikuwepo wakati wa uhamisho huo.
"Pia tunahitaji kuwasaidia walinzi wa mazingira kulinda mimea na wanyama wetu," Bi Nabintu aliiambia TRT Afrika.
Hifadhi ya Kitaifa ya Garamba Iliyoundwa mnamo 1938, ni moja ya mbuga kongwe zaidi barani Afrika. Lakini migogoro, ujangili na ukosefu wa usalama wa kudumu katika eneo tete la Kongo vimeangamiza wanyamapori wake kwa miaka mingi.
Kulingana na Hazina ya Wanyamapori Ulimwenguni, ''mwanzoni mwa karne ya 20, faru 500,000 walizurura Afrika na Asia. Kufikia mwaka wa 1970, idadi ya faru ilishuka hadi 70,000, na leo hii, karibu faru 27,000 wamesalia porini.''
Huku faru weupe zaidi wa kusini wakitarajiwa kufikishwa katika Hifadhi ya Taifa ya Garamba siku zijazo, wachambuzi wanasema hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kukabiliana na tatizo la uwindaji.
Wawindaji haramu kwa kawaida huwalenga wanyama pori kwa ajili ya sehemu zao ambazo husafirishwa nje ya nchi. Ni muhimu katika mchakato wa virutubisho vya chakula, vipodozi na katika dawa za asili na za kisasa.
Shughuli nyingine za kibinadamu kama vile ukataji miti na uchomaji misitu zimeharibu makazi asilia ya wanyama. Mkurugenzi Mtendaji wa African Parks, Peter Fearnhead, alisema juhudi za kuwaokoa faru weupe katika Mbuga ya Kitaifa ya Garamba nchini DRC "zimechelewa sana"
Lakini alikuwa na matumaini kwamba kuletwa upya kwa faru hivi karibuni ''ni mwanzo wa mchakato ambapo faru mweupe wa kusini, ataweza kujaza nafasi ya faru mweupe wa kaskazini katika mazingira hayo.''