Mamia ya watu walikusanyika katika kitovu cha riadha nchini Kenya cha Eldoret kwa msafara wa mazishi ya nyota wa mbio za marathon Kelvin Kiptum, aliyefariki mapema mwezi huu katika ajali ya gari.
Jeneza lake, lililozungushiwa maua, lilibebwa kwenye gari la kubebea maiti kupitia barabara za mji huo katika Bonde la Ufa magharibi mwa Kenya, siku ya Alhamisi, wengine wakiangalia msafara huo kwa majonzi, huku wengine wakiimba za kuomboleza.
Kiptum alifariki Februari 11, akiwa na umri wa miaka 24, miezi michache tu baada ya kuvunja rekodi ya dunia ya mbio za marathon.
"Ni vigumu kukubali hili lilifanyika. Ni pengo kubwa katika riadha ya Kenya," mwanachama wa kamati kuu ya Riadha Kenya Barnaba Korir alisema.
Maandamano hayo yalipitia barabara zenye mashabiki na wanariadha wakati ikielekea Iten, eneo la mafunzo ya spoti kwa wanariadha.
"Lazima tukubali kwamba Kiptum hayuko nasi tena," kasisi Philip Chumo alisema huku jeneza likipakiwa kwenye gari nyeusi la kubebea maiti.
Polisi walisema Kiptum alikuwa akiendesha gari karibu na Eldoret mwendo wa tano za usiku , gari lake lilipotoka barabarani hadi kwenye mtaro na kugonga mti.
Kocha wake Mnyarwanda, Gervais Hakizimana, 36, pia alifariki katika ajali hiyo, huku abiria mwengine ambaye ni mwanamke akijeruhiwa.
Kiptum aliingia katika mbio za marathon mnamo 2022 na kuvunja rekodi ya ulimwengu huko Chicago Oktoba mwaka jana.
Alikimbia kwa muda wa saa mbili, sekunde 35, akipunguza sekunde 34 kutoka kwa rekodi ya mwanzo iliyowekwa na gwiji wa mbio za marathon wa Kenya Eliud Kipchoge.
Mwanariadha huyo mchanga alikuwa ameshiriki katika mbio za marathoni tatu pekee na kurekodi mara saba mbio za haraka zaidi katika mashindano hayo.
Ndiye aliyepewa nafasi kubwa ya kutwaa medali ya dhahabu kwenye Michezo ya Olimpiki ya mwaka huu ya Paris, ambapo alitarajiwa kupambana na Kipchoge kwa mara ya kwanza.
Kiptum, ambaye alikuwa na mke na watoto wawili, atazikwa Ijumaa nyumbani kwake Chepkorio, Eldoret.