Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) lafafanua kuhusu ndege yake iliyoko Malaysia

Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) lafafanua kuhusu ndege yake iliyoko Malaysia

Hii inafuatia hatua ya kutoonekana kwa ndege ya aina ya Dreamliner 787-7, kwa takribani miezi saba.
Moja ya ndege zinazomilikiwa na ATCL./Picha: Wengine

Kukaa kwa muda mrefu kwa ndege ya ATCL aina ya Dreamliner 787-7 katika karakana huko Malaysia, kunatokana na uhaba wa injini za ziada.

Katika taarifa yake kwa umma, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limesema kuwa kukaa kwa muda mrefu kwa ndege yake ya Dreamliner 787-8, kunatokana na uhaba wa injini za ziada ambazo zingeweza kutumika wakati injini zake zikifanyiwa matengenezo.

"Ndege za Boeing 787-8 za ATCL hutumia injini za Kampuni ya Rolls Royce aina ya Trent 1000. Kwa mujibu wa miongozo ya Mamlaka za Usafiri wa Anga na watengenezaji wa injini hizo, imekuwa ni lazima kufanyiwa matengenezo makubwa, kila baada ya miruko 1000," imesomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa ATCL, hii ni baada ya kugundulika kwa matatizo ya kisanifu katika mifumo ya ufuaji wa nguvu wa kuendesha ndege, kwa injini nyingi za matoleo mapya.

Shirika hilo, limeongeza kuwa matatizo ya namna hiyo yamesababisha kutolewa kwa miongozo maalum kuhusu uchunguzi wa injini wa mara.

"Injini hizo zinapopelekwa kwa matengenezo zinalazimika kuzingatia kufuata zamu kutokana na idadi kubwa ya injini zinazosubiria matengenezo na hivyo kupelekea kuchukua muda mrefu kuhitimisha matengenezo yake," taarifa hiyo imeongeza.

Kulingana na ATCL, ndege hiyo inatarajiwa kuwasili kutoka Kuala Lumpur, mwezi Juni 2024.

TRT Afrika