Mkuu wa Huduma ya Utumishi wa Umma nchini Kenya Felix Koskei ameongoza mkutao wa mashirika ya serikali kutatua mgomo wa madaktari ambao umeingia siku ya tisa Ijumaa.
Hii ni kufuatia agizo la Mahakama ya Kazi na Ajira kushughulikia masuala ya kudumu ya uhusiano wa wafanyakazi katika sekta ya afya.
Muungano wa Madaktari, Wafamasia na Madaktari wa Meno nchini Kenya, KPMDU, ulitoa notisi kwa serikali ya kuanza kwa mgomo kuanzia Machi 13, 2024, iwapo serikali itashindwa kutatua changamoto zao.
Madaktari hao wanaitaka serikali kutoa ajira kwa wanafunzi wahudumu wa afya mara moja na kulipa malimbikizo ya mishahara ya madaktari kulingana na Makubaliano ya Pamoja ya 2017.
"Tunahimiza madaktari kufikiria upya uamuzi wao na wakubali kurudi kwenye meza ya mazungumzo tuone jinsi tutaweza kuwapa ajira wale madaktari waliomaliza mafunzo," Mkuu wa Huduma ya Utumishi wa Umma nchini Kenya Felix Koskei amesema baada ya mkutano wao.
Wahudumu hawa wamepuuza tishio la Waziri wa Afya aliyewaonya kuwa wanaweza kupoteza ajira iwapo wataendelea na mgomo.
"Na pia ni lazima tukubaliane kwa idadi tunayoweza kwa ajili ya kuwapa malipo madaktari 1200 wanaongojea nafasi. Lakini lazima ujumbe uwe wazi kuwa serikali iko makini kuhakikisha kuwa madaktari wote wanaofuzu masomo wanapewa nafasi kutumia ujuzi wao na kufanya kazi katika hospitali," Koslei ameongezea.
" Kile ambacho kitatuchukua siku moja au mbili kutatua ni idadi na ni lini wanafaa kupewa nafasi katika hopsitali."
Amesema waajiri wasiwachukulie hatua yoyote madaktari ambao hawajaenda kazini kwa sababu ya kuunga mkono mgomo huo.