Mjadala wa kuundwa upya kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC umevuma nchini Kenya huku baadhi ya wananchi wakisema Rais William Ruto anafanya makusudi kutounda Tume hiyo.
Kenya haijakuwa na wakala wa uchaguzi unaofanya kazi kikamilifu, miaka miwili tangu kuondoka kwa Tume iliyopita.
Kukosekana kwa makamishna kunaifanya Tume ya IEBC kushindwa kutekeleza majukumu yake muhimu, ambayo ni pamoja na uwekaji wa mipaka na kusimamia uchaguzi mdogo.
Hata hivyo, Naibu Rais wa Kenya Kithure Kindiki amesema serikali haina lawama.
Kindiki amezitaka pande zinazohusika katika mvutano wa kisheria kuhusu kuundwa upya kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kufikia suluhu nje ya mahakama.
"Nimeona baadhi ya watu wakilaumu serikali," Kindiki alisema.
“Hii ni nchi inayoongozwa na sheria. Sheria ikiwepo, Serikali haina uwezo wa kufanya chochote. Kwa hivyo, tunaomba waliowasilisha kesi hizo waafikiane nje ya mahakama ili tuendelee na uundaji upya wa IEBC.”
Hii inafuatilia matamshi wa aliyekuwa makamu wa rais Rigathi Gachagua aliyesema ukosefu wa makamishna wa Tume ya Uchaguzi unatia doa katika uaminifu wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
"Uchaguzi unaaminika kama mchakato muhimu. Ripoti ya Krigler ilipendekeza Tume ya Uchaguzi iwepo miaka mitatu kabla ya uchaguzi. Sasa tuna takriban miaka 2 na nusu bila IEBC na watu wanaweza kusoma ufisadi,” amesema DP huyo wa zamani.
Katika hafla tofauti, kiongozi wa Chama cha Wiper Kalonzo Musyoka pia aliwakashifu Rais William Ruto na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula kwa 'kuchelewesha' uundaji wa IEBC.
"Nchi kama yetu inawezaje kujisimamia ikiwa hatuna Tume ya Uchaguzi? Uchaguzi Mkuu ni 2027, hii ni 2024, ni lini Tume hii itaundwa?” aliuliza.
Kalonzo alidai kuwa Serikali, kupitia wawakilishi, ilihamia kortini kumzuia kiongozi wa chama cha Azimio Koki Muli aliyetaka kuwa sehemu ya jopo linalopaswa kuunda upya IEBC.
Kuna vikwazo vya kisheria ambavyo vimekuwa changamoto katika kutekelezwa kwa jopo la uteuzi wa IEBC.
Kumekuwa na vuta ni kuvute kuhusu nani anafaa kuwa katika jopo, huku upinzani ukitanguliza majina tofauti. Upinzani chini ya Muungano wa Azimio la Umoja umekumbwa na mizozo kuhusu mwakilishi halali wa vyama vidogo kwenye jopo hilo.
Sheria inasemaje?
Kulingana na katiba ya Kenya Tume huru ya Uchaguzi, IEBC, inafaa kuwa na mwenyekiti na wajumbe wengine sita watakaoteuliwa kwa mujibu wa Ibara ya 250(4) ya Katiba na masharti ya Sheria hii.
Wajumbe wa Tume wanateuliwa kwa muhula mmoja wa miaka sita na hawatastahili kuteuliwa tena baada ya zoezi la uchaguzi kukamilika. Wajumbe hao watahudumu kwa muda wote.
Angalau miezi sita kabla ya mwisho wa muda wa mwenyekiti au mjumbe wa Tume au ndani ya siku kumi na nne baada ya kutangazwa kwa nafasi ya mwenyekiti au mjumbe wa Tume kwa mujibu wa Katiba au Sheria hii, Rais atateua jopo la uteuzi linalojumuisha watu saba kwa madhumuni ya uteuzi wa mwenyekiti au mjumbe wa Tume.
Jopo la uteuzi, ndani ya siku saba baada ya kuteuliwa, litaalika maombi kutoka kwa watu wenye sifa na kuchapisha majina ya waombaji wote na sifa zao kwenye Gazeti la Serikali.
Rais, ndani ya siku saba baada ya kupokea majina yaliyoidhinishwa na Bunge, kwa notisi kwenye Gazeti la Serikali, atateua Mwenyekiti na wajumbe wa Tume.