Serikali ya Kenya inawahakikishia uwajibikaji kamili kwa wote ambao walihusika au kuchangia katika ajali ya moto katika Shule ya Hillside Endarasha Academy huko Kieni Magharibi, Kaunti ya Nyeri, ambayo umesababisha vifo vya watu 17.
"Asubuhi ya leo, Kenya iliamka na kusikia habari za kuhuzunisha za kufiwa na kujeruhiwa vibaya kwa watoto wa Kieni Hillside Academy katika Kaunti ya Nyeri kutokana na moto mbaya wa kabla ya alfajiri ambao uliteketeza bweni la wanafunzi hao walipokuwa wamelala," Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki amesema katika akaunti yake ya X.
Waziri huyo alitembelea shule hiyo.
"Kufuatia agizo la Rais William Ruto mapema leo, mashirika yote husika ya Serikali yametumwa na kuagizwa kukusanya kila msaada na usaidizi unaowezekana kwa familia zilizoathiriwa ... kutafuta ukweli kuhusu kilichosababisha moto huo na kusababisha hasara na kujeruhiwa kwa familia hiyo na vijana wengi," Kindiki alisema.
Mapema Ijumaa Rais William Ruto aliahidi kuwa waliohusika na tukio hilo watasakwa.
“Naagiza mamlaka husika kuchunguza kwa kina tukio hili la kutisha, waliohusika watawajibishwa, Serikali chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Uratibu wa Serikali ya Kitaifa inakusanya rasilimali zote muhimu ili kusaidia familia zilizoathirika,” aliongeza," Rais Ruto alisema.
"Wanafunzi waliojeruhiwa vibaya wamekimbizwa katika Hospitali ya Kanisa la Mathari na Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Nyeri kwa ajili ya matibabu," alisema Msemaji wa Serikali ya Kenya Isaac Maigua Mwaura katika taarifa yake.
"Bweni lililoathiriwa lilikuwa na wavulana kutoka darasa la 4 hadi 8. Jumla ya wavulana 156 walikuwa wakilala katika bweni hilo," Mwaura alisema.
Aliongeza kuwa maafisa wa huduma za dharura bado hawajatangaza idadi ya mwisho ya waliofariki.