Rais wa Kenya William Ruto amewajibu maaskofu wa kanisa la Katoliki ambao wameilaumu serikali kwa kukosa kutimiza wajibu kwa wananchi na kuwataka wawe wa kweli.
Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya (KCCB), Askofu Mkuu Maurice Muhatia, Alhamisi aliwaongoza maaskofu katika kuikosoa wazi serikali ya Rais William Ruto kuwa imeshindwa kutimiza ahadi zake za uchaguzi, pamoja na kushindwa kusikiliza kilio cha watu wa kawaida na kuirudisha Kenya katika mafanikio ya kidemokrasia.
"Sisi sote tumeunganishwa katika huduma ya watu. Ndiyo maana tunafanya kazi na viongozi wote - pamoja na makasisi - kuelekea Kenya ambayo sote tunaweza kujivunia," Rais William Ruto alisema katika sherehe ya kuhitimu kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tangaza jijini Nairobi.
"Lakini hata tunapotafuta kuwajibishana, lazima tujitahidi kujengana kwa ukweli," Rais Ruto amesema.
Taarifa ya maaskofu imezua majadiliano nchini huku ikizua wingu jipya ya wananchi kuilaumu serikali ya Rais Ruto.
“Utamaduni wa uongo unachukua nafasi ya uadilifu na heshima ambayo Wakenya wanastahili. Kimsingi, inaonekana kwamba ukweli haupo, na kama upo, ni kile tu ambacho serikali inasema,” Askofu Mkuu Muhatia alisema.
“Kwa bahati mbaya, inaonekana Wakenya wamevumilia uongo ambao wanaambiwa kila mara na wanasiasa. Wakenya lazima wajifunze kutopongeza au kuhalalisha uongo ambao wanasiasa wanawaambia, lakini wanapaswa kuamua kutafuta na kuongozwa na ukweli,” aliongezea.
Maaskofu walitaja sekta kama vile ya elimu, afya na usalama kuwa kati ya zilizoathirika vibaya.
Awali walipinga kuanzishwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Ushuru wa 2024.
Serikali yajitetea
Wizara tofauti za serikali nchini Kenya zimejitokeza kujibu madai ya Muungano wa Maaskofu hao kuwa serikali haijatimiza kikamilifu wajibu wake kwa wananchi.
Maaskofu wanadai katika taarifa yao kuwa huku serikali ya Rais Willim Ruto ikifanya mabadliko katika mfumo wa bima ya afya, mashirika ya imani ambayo yako na huduma za imani yanadai mabilioni ya malipo.
Wizara ya afya imekana madai haya
Imeelezea kuwa kufikia Oktoba 4, 2024, mfumo unaoondolewa wa NHIF ulikuwa na deni ya bilioni 1 ya mashirika tofauti ya afya.
"Serikali ina nia ya kumaliza kulipa deni hii," Wizara ya Afya imejibu katika taarifa.
Imesema mfumo wa NHIF ulikuwa na kandarasi na vituo vya afya 8886, vikiwemo vya umma na vile vya binafsi. Imesema mashirika ya kidini yalikuwa na vituo 312 ambayo inawakilisha 3.5% ya wakadarasi wote.
Imesema serikali kupitia mfumo mpya wa afya itamaliza malipo ya deni hilo wiki ijayo lenye thamani ya shilingi 2.5 bilioni.
Sekta ya Elimu
Maaskofu walikosoa mabadiliko ya mfumo wa elimu, ikiwa sasa Kenya imeanza mfumo unaoitwa 'competency-based curriculum , CBC' .
Hapo awali wanafunzi walisoma miaka 8 ya shule ya msingi, miaka 4 ya sekondari, na miaka 4 ya elimu ya chuo kikuu ya shahada ya kwanza.
Hivi sasa, katika mfumo wa CBC wanafunzi wanasoma miaka 6 ya shule ya msingi, miaka 3 ya sekondari ya chini, miaka 3 ya sekondari ya juu, na miaka 4 ya elimu ya chuo kikuu ya shahada ya kwanza.
Maaskofu wamekashifu mfumo huo kwamba unaanguka.
Wizara ya Elimu imejibu
"Mfumo wa CBC ulianza 2017 na una lengo la kuwainua wanafunzi katika sekta tofauti ikiwemo sayansi na teknolojia..." imesema utekelezaji huo unafuata utafiti wa kina uliofanyika.
Usalama Nchini
Maaskofu pia wamelaani ongezekao la mauaji na utekwaji nyara nchini kati ya changamoto nyengine za usalama.
Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya DCI, imewajibu kwa kuelezea visa tofauti ambavyo bado inavifuatilia.
"Huduma ya Taifa ya Polisi inawahakikishia wananchi kuwa tumeongeza usalama katika sehemu zote nchini na tunaendelea kuomba wananchi washirikiane nasi kwa kutoa maelezo yoyote ambayo yanaweza kusaidia katika uchunguzi," taarifa ya DCI imesema.