Senegal siku ya Jumapili iliadhimisha kumbukumbu ya miaka 80 ya mauaji ya wanajeshi wa Kiafrika waliopigania Ufaransa wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, na waliuawa kwa kupigwa risasi na wanajeshi wa Ufaransa mwaka 1944 kwa kudai kutendewa haki na malipo waliporejea.
Nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa muda mrefu imekuwa ikimtaka mkoloni wake wa zamani kuwajibika, kuomba radhi rasmi na kuchunguza ipasavyo mauaji yaliyotokea huko Thiaroye, kijiji cha wavuvi nje kidogo ya mji mkuu wa Senegal, Dakar.
Maadhimisho hayo, ambayo yalifufua madai haya, yalifanyika wakati Ufaransa ikipoteza ushawishi kwa makoloni yake ya zamani ya Afrika, ambayo mengi yamegeukia Urusi kwa usalama badala yake.
"Wapiganaji wa Kiafrika walijitolea kwa kila kitu. Walitoa ujana wao, walitoa damu yao, walitoa nyama yao kwa ajili ya uhuru na amani ya dunia," Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye aliwaambia wageni na waandishi wa habari.
Kumbukumbu za mauaji hayo zinatofautiana, sawa na idadi ya waliouawa, ambayo rais wa zamani wa Ufaransa Francois Hollande aliiongeza hadi takriban 70 kutoka 35 wakati wa ziara yake mjini Thiaroye mwaka 2014.
Wanahistoria wanasema huenda mamia walikufa katika makabiliano na mamlaka ya kikoloni.
Sherehe hiyo ambayo waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa alihudhuria pamoja na wakuu wengine wa nchi za Afrika, ilianza kwa kutembelea makaburi ya kijeshi ya Thiaroye kuweka maua.
Mwongozo uliochapishwa wa sherehe hiyo ulielezea "ukandamizaji wa kutisha" wa wanajeshi wa kitengo cha Waafrika wa Senegal, ambao walizingirwa na kupigwa risasi kwa kuomba fidia inayostahili.
Siku chache kabla ya maadhimisho hayo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliandika barua kwa umma kwa mwenzake wa Senegal Faye ambapo alitaja mauaji hayo kuwa "mauaji".
Faye alisema kukiri kwa Macron ni hatua muhimu katika mchakato wa kurejesha heshima na utu wa waathiriwa.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot alisema katika hotuba yake nchi yake imetambua kuwa siku hiyo, "msururu wa matukio ulianzishwa na kusababisha mauaji".
Gaspard Mbaye, mkuu wa chama kinachojishughulisha na kumbukumbu za wanajeshi hao, aliambia Reuters kuwa amesikitishwa kwa sababu alitarajia zaidi kutoka kwa serikali ya Ufaransa.
"Wanaendelea kuficha ukweli na kujaribu kuwapumbaza watu," Mbaye alisema.