Watawala wa kijeshi wa Niger wamekaribisha tangazo kwamba Ufaransa itawaondoa wanajeshi wake nchini humo mwishoni mwa mwaka kama "hatua mpya kuelekea uhuru".
Kauli hiyo imekuja saa chache baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kutangaza kwamba hivi karibuni Paris itamuondoa balozi wake kutoka Niger, ikifuatiwa na kikosi chake cha kijeshi katika miezi ijayo.
"Jumapili hii, tunasherehekea hatua mpya kuelekea uhuru wa Niger," ilisema taarifa ya watawala wa kijeshi wa nchi hiyo, walionyakua mamlaka mwishoni mwa Julai kwa kumpindua Rais Mohamed Bazoum mnamo Julai 26.
Kumekuwa na maandamano yanayoongezeka ya maelfu ya raia wa Niger wanaounga mkono mapinduzi wakitaka kuondoka kwa vikosi vya Ufaransa ambavyo vimekuwa vikishiriki katika kampeni ya kupambana na ugaidi katika eneo la Sahel kwa miaka mingi.
Marufuku ya ndege za Ufaransa
"Wanajeshi wa Ufaransa na balozi wa Ufaransa wataondoka katika ardhi ya Niger ifikapo mwisho wa mwaka," iliongeza taarifa hiyo kwenye televisheni ya taifa.
"Huu ni wakati wa kihistoria, ambao unazungumzia dhamira na mapenzi ya watu wa Niger," junta ilisema.
Mapema Jumapili, kabla ya tangazo la Macron, chombo kinachosimamia usalama wa anga barani Afrika (ASECNA), kilitangaza kuwa watawala wa kijeshi wa Niger wamepiga marufuku "ndege za Ufaransa" kuruka juu ya anga ya nchi hiyo.
Ufaransa ina wanajeshi 1,500 nchini Niger. Haijabainika haswa iwapo watahamishwa hadi Ufaransa au nchi nyingine barani Afrika.
Macron alisema Ufaransa, nchi yenye nguvu ya zamani ya kikoloni nchini Niger, haitajiruhusu "kushikiliwa mateka na watukutu".
Ushawishi wapungua
Kujiondoa kwa Ufaransa, ambako kunakuja baada ya wiki za shinikizo kutoka kwa junta na maandamano ya kuwaunga mkono, kunaweza kuzidisha wasiwasi wa Magharibi juu ya ushawishi unaoenea wa Urusi barani Afrika. Kikosi cha mamluki cha Urusi Wagner tayari kipo katika jirani ya Niger ya Mali.
Rais wa Ufaransa amekataa kutambua serikali ya kijeshi kama mamlaka halali ya Niger lakini akasema Paris itaratibu kuondoka kwa wanajeshi hao pamoja na viongozi wa mapinduzi.
Ushawishi wa Ufaransa juu ya makoloni yake ya zamani umepungua katika Afrika Magharibi katika miaka ya hivi karibuni.
Vikosi vyake vimefurushwa nje ya nchi jirani za Mali na Burkina Faso tangu mapinduzi katika nchi hizo, na kupunguza jukumu lake katika mapambano ya kanda nzima dhidi ya uasi mbaya wa wapiganaji wanaohusishwa na Al Qaeda.
Hadi mapinduzi hayo, Niger ilikuwa imesalia kuwa mshirika mkuu wa usalama wa Ufaransa na Marekani, ambazo zimeitumia kama ngome ya kupambana na waasi katika eneo la Sahel la Afrika Magharibi na Kati.