Samora Machel: Shujaa dhidi ya ukoloni aliyekufa kwa ajali ya ndege

Samora Machel: Shujaa dhidi ya ukoloni aliyekufa kwa ajali ya ndege

Rais huyo wa kwanza wa Msumbiji anatajwa kuwa shujaa wa ukombozi wa nchi hiyo.
Samora Machel alifariki dunia kwa ajali ya ndege mwaka 1986./Pciha: Getty

Na Susan Mwongeli

TRT Afrika, Istanbul, Uturuki

Miaka 38 baada ya kifo chake, bado jina la Samora Machel linaendelea kuvuma katika eneo la kusini mwa Afrika alama ya ukombozi dhidi ya ukoloni.

Akiwa amezaliwa Septemba 29, 1933 huko Chilembene nchini Msumbiji, maisha ya awali ya Machel yaliakisi mtu jasiri na shupavu ambaye baadaye alikuja kuwa mwiba mkali dhidi ya ukoloni.

Machel, ambaye alikuja kuwa Rais wa Msumbiji baada ya nchi hiyo kupata uhuru wake, alikuwa ni kati ya viongozi wenye maono barani Afrika, wakiwemo na akina Patrice Lumumba wa DRC na Thomas Sankara wa Burkina Faso.

Machel na mawaziri wengine walipoteza uhai kufuatia ajali ya ndege iliyotokea nchini Afrika Kusini Oktoba 19, 1986 wakiwa safarini kuelekea Maputo, wakitokea nchini Zambia.

Wengi wanaamini kuwa utawala wa kibaguzi wa nchini Afrika Kusini ndio uliohusika na ajali hiyo.

Machel alipoteza ndugu zake wakati wa utawala wa kibaguzi wa kireno mwenye miaka ya 1950.

Alikuwa kijana tu kwa wakati huo. Alivuka viunzi mbalimbali na kukiongoza chama cha Frelimo dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ureno. Machel aliiongoza Msumbiji kupata uhuru wake mwezi Juni 1975.

Mtandao wa upinzani

Kama Rais wa kwanza wa Msumbiji, Machel aliweka kipaumbele chake katika elimu, huduma ya afya na mageuzi kwenye masuala ya ardhi na kufanikiwa kutengeneza nchi ya kijamii.

Samora Machel alianzisha mapambano baada ya ndugu zake kupotezwa wakati wa utawala wa kikoloni./Picha: Getty

Machel alijitahidi sana kuigeuza nchi ya Msumbiji iwe ni ya kujitegemea.

Ushawishi wa Machel umevuka mipaka ya Msumbiji, huku akitajwa kuwa ni tumaini la watu walioonewa kusini mwa Afrika.

Atakumbukwa kwa kuwapa hifadhi wapigania uhuru kutoka nchi za Zimbabwe, Afrika Kusini na Angola na kufanikiwa kutengeneza mtandao imara dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukoloni.

Ushawishi wa Machel umevuka mipaka ya Msumbiji, huku akitajwa kuwa ni tumaini la watu walioonewa kusini mwa Afrika./Picha: Getty

Urithi wa Machel unadumu, na kutia moyo vizazi kupigania uhuru na haki.

TRT Afrika