Kiongozi wa timu ya uangalizi wa uchaguzi wa nchini Mauritius (SEOM), Jaji Mstaafu wa Tanzania Mohammed Chande Othman, amezindua rasmi timu hiyo siku chache kabla ya kuanza kwa Uchaguzi Mkuu nchini Mauritius.
Akizindua rasmi timu hiyo jijini Port-Louis nchini Mauritius ,Jaji huyo Mkuu Mstaafu wa Tanzania amewataka wadau mbalimbali watakaoshiriki mchakato huo kuheshimu majukumu ya chombo hicho, kamba ilivyokasimiwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
"Kwa kuzingatia hali ya amani nchini Mauritius, na baada ya kufanya uhakiki wetu, ni wazi kuwa nchi hii iko tayari kwa kufanya uchaguzi," amesema Chande katika taarifa yake.
Pia, ameongeza kuwa timu yake itatoa taarifa yake awali siku ya Novemba 12, 2024, siku mbili baada ya kufanya uchaguzi.
"Dhamira yetu siyo tu kuangalia uchaguzi, bali ni kuchangia kwa njia ya kujenga, huku tukifanya tathmini ya kina kama uchaguzi unazingatia viwango vya kidemokrasia," alisema Chande.
SEOM, ambayo ilianza kazi zake za maandalizi ya usimamizi wa uchaguzi nchini humo mnamo tarehe 28 Oktoba, inajumuisha waangalizi 73, kutoka nchi nane wanachama wa SADC.
Uchaguzi wa Mauritius, utakaofanyika Novemba 10, ni sehemu ya mfululizo michakato ya kuchagua viongozi unaondelea kufanyika kwenye nchi wanachama saba wa SADC, ambayo ni jumuiya yenye watu wapatao milioni 130.