Zimbabwe imepokea tani 1,000 za unga wa mahindi kutoka Rwanda katika mapambano yake dhidi ya ukame unaosababishwa na El Niño.
Rwanda inasema ilitoa unga huo kusaidia jamii zilizoathirika nchini Zimbabwe, kuitikia wito wa Rais Emmerson Mnangagwa wa msaada wa chakula.
Hatua hii inajiri baada ya Mnangagwa kutangaza msimu wa kilimo wa majira ya joto wa 2023-24 kuwa hali ya maafa kutokana na ukame.
Mjumbe mkuu wa Rwanda nchini Zimbabwe, James Musoni, alikabidhi shehena hiyo mjini Harare, akisisitiza dhamira ya nchi yake kuiunga mkono Zimbabwe.
Kusimama pamoja
"Kama nchi za Afrika, tunapaswa kusimama pamoja katika nyakati nzuri na ngumu," Musoni alisema.
Ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili ni mkubwa, huku Mikataba kadhaa ya Maelewano (MOUs) ikitiwa saini, kuonesha uhusiano wao thabiti.
"Hii ndiyo roho ya Ubuntu ambayo Rwanda imedhihirisha kwa kuitikia wito wa kimataifa wa Mheshimiwa Rais Mnangagwa kufuatia ukame uliosababishwa na El Nino. Daima, Zimbabwe itakumbuka mchango na ukarimu wenu.
"Tutahakikisha mchango huo unawafikia jamii zinazostahili,” alisema Daniel Garwe, ambaye ni Waziri wa Serikali za Mitaa.
Hali ya El Niño imeleta hali mbaya ya ukame nchini Zimbabwe, na kuzidisha uhaba wa chakula na upungufu wa lishe. Huku zaidi ya watu milioni 7.6 wakiwa katika hatari ya kukumbwa na njaa kali, usaidizi huu ni wa wakati unaofaa na muhimu.