Hali ya joto kupita kiasi imeenea katika nchi tofauti barani / Picha: AP

Rwanda imeripoti joto jingi kuliko kawaida katika maeneo mbalimbali ya nchi yake.

Shirika la Hali ya Hewa la Rwanda linasema kuanzia Machi 11 hadi Machi 20 maeneo kadhaa yalishuhudia kati ya nyuzi joto 20 hadi 30, ikiwa ni kiwango cha juu kidogo ya wastani wa joto la muda mrefu.

Maeneo mengi ya Jiji la Kigali, Wilaya za Bugesera na Nyagatare, eneo la Amayaga, bonde la Bugarama, na maeneo katika wilaya za Ngoma na Gatsibo yamekabiliwa na kiwango cha joto cha juu zaidi kati ya 28°C na 30°C.

Hali hii ya joto kupita kiasi pia imeshuhudiwa katika nchi tofauti barani Afrika.

Kwa mfano Sudan Kusini imelazimika kufunga kwa muda usiojulikana taasisi zote za masomo kuanzia Jumatatu, Machi 18 kutokana na wimbi la joto linaloendelea kushuhudiwa Afrika Mashariki.

Wizara ya Afya na Elimu imewashauri wazazi kuwaweka watoto wote ndani kwani joto kali linatarajiwa kuongezeka hadi 45°C (113F). Hali ya hewa ya joto sana inatarajiwa kudumu angalau wiki mbili.

Wanasayansi wanasema hali hii ya joto kupita kawaida ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi duniani.

TRT Afrika