Wanafunzi wanaoonyesha dalili za Marburge lazima wapelekwe katika kituo cha afya mara moja/  Picha:  Wizara ya Elimu Rwanda  X

Wizara ya Elimu nchini Rwanda imesitisha kwa muda ziara za kila mwezi kwa wanafunzi katika shule za mabweni ikiwa ni moja wapo ya hatua za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa homa ya Marburg (MVD), ugonjwa hatari wa kuvuja damu.

Taarifa ya Oktoba 2 kutoka Wizara ya Afya inaonyesha kuwa ugonjwa huo ulikuwa tayari umegharimu maisha ya watu 11.

"Ili kupunguza usambazaji, imesimamisha kuwatembela watoto shuleni kila mwezi," taarifa kutoka Wizara ya Elimu imesema.

Serikali imesema watoto utaratibu huo utaanza tena baada ya tathmini ya Wizara na Mamlaka ya Afya.

"Katika hali za dharura, wazazi wanaweza kushirikiana na wasimamizi wa shule kutuma vifaa muhimu kupitia mbinu mbadala, ikiwa ni pamoja na njia za kidijitali inapowezekana," taarifa kutoka Wizara ya Elimu iliongezea.

Kulingana na miongozo mipya, wasimamizi wa shule na walimu lazima wafuatilie wanafunzi iwapo watakuwa na dalili za ugonjwa wa Marburg, ambazo ni pamoja na homa kali, maumivu makali ya kichwa, maumivu ya misuli, uchovu, kichefuchefu, kutapika na kuharisha.

Wanafunzi wanaoonyesha dalili hizi wanatakiwa kupelekwa kwenye kituo cha afya mara moja.

"Kufuatia maagizo kutoka kwa Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu imetoa hatua za kuzuia kutumika katika shule zote hadi taarifa nyingine," ilisoma sehemu ya taarifa hiyo.

Wazazi pia wametarajiwa kutekeleza jukumu lao.

Ikiwa mtoto anaonyesha dalili zozote, imebainika, lazima awekwe nyumbani na kupelekwa kituo cha afya kwa tathmini.

Wanafunzi wanapaswa kurudi shule baada ya kupata kibali kutoka kwa mtaalamu wa afya. Miongozo hiyo pia inabainisha kuwa wanafunzi wote lazima wazingatie hatua za kuzuia ili kusaidia kukomesha kuenea kwa virusi.

TRT Afrika