Ekiru alipimwa na kukutwa na vitu vilivyopigwa marufuku katika sampuli zake za mkojo/ Picha: AFP

Mwanariadha wa Kenya Titus Ekiru amepigwa marufuku kwa miaka kumi na Kitengo cha Uadilifu wa Riadha (AIU) kwa madai ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Ekiru anashutumiwa kwa kushirikiana na daktari wa ngazi ya juu katika hospitali ya Kenya ambaye alimsaidia mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 31 kuharibu sampuli ili kuzuia uchunguzi wa AIU.

AIU ilisema kwamba Ekiru alipimwa na kukutwa na vitu vilivyopigwa marufuku katika sampuli zake za mkojo wakati wa mashindano ya Generali Milano Marathon mnamo Mei 16, 2021, na Marathon ya Abu Dhabi mnamo Novemba 26, 2021, ambazo alishinda.

Zawadi zimerudishwa

Mwenyekiti wa AIU David Howman alitangaza marufuku hiyo, akiongeza kwamba sasa wanafanya kazi na maafisa wa serikali na mashirika ya riadha "kufichua matumizi ya dawa za kusisimua misuli katika riadha ya Kenya na kufichua mitandao ambayo inaweza kuhusika."

"Kwa wanariadha wanaohusika na doping na wasaidizi, wanaowasaidia, kuna ujumbe mmoja mkali kutoka kwa kesi hii - hakuna mahali pa kujificha."

Mbali na marufuku - ambayo itaanza Juni 28, 2022 (tarehe ya kusimamishwa kwa muda kwa Ekiru) hadi Juni 27, 2032 - matokeo ya ushindi ya Ekiru tangu Mei 16, 2021, yamebatilishwa, na kusababisha kunyang'anywa zawadi na pesa zote.

TRT Afrika