Real Madrid ya Hispania ndio mabingwa wapya wa nchi hiyo baada ya kuifunga Cadiz, mabao 3-0 bila katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Santiago Bernabéu, Mei 4, 2024.
Vijana wa Carlo Ancelotti wametwaa taji la La Liga kwa mara ya 36, huku michezo minne ikisalia kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo.
Mabao yaliyotiwa kimiani na Brahim Díaz, Jude Bellingham na José Luis Mato Sanmartín, maarufu kama Joselu, yalitosha kuipa Real Madrid alama 87, kabla ya kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa La Liga.
Hata hivyo, iliwalazimu Real Madrid kusubiria hatma ya mchezo kati ya Girona na Barcelona ili waanze sherehe zao za ubingwa katika viunga vya Madrid.
Katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Municipal de Montilivi, siku hiyo hiyo, Barcelona ilikubali kichapo cha mabao 4-2, na hivyo kusalimisha taji la La Liga kwa Real Madrid.
Matokeo hayo yanaipa nafasi Girona, timu ndogo kutoka Katalunya, kushiriki michuano ya Ulaya, msimu ujao.
Ikumbukwe pia, Girona imeshiriki ligi kuu ya Hispania kwa mara ya nne, katika historia yao.