Jude Bellingham, wa England na Real Madrid, atunukiwa Golden Boy. Picha: Real Madrid

Bellingham, alitunukiwa tuzo hiyo ya kifahari ya Golden Boy inayomtambua mchezaji wa kiume mwenye maonyesho bora zaidi ya mchezo.

Kiungo huyo wa Madrid aliibuka na asilimia 97% ya kura za waandishi wa habari 50 wa spoti, ambao walichagua kutoka orodha ya wachezaji 25, akiwemo mwenzake wa Madrid, Arda Güler.

Tuzo hizo, zilizofanyika Turin, Italia, zinajiri kufuatia ushindi wa taji la Kopa alilibeba Bellingham kwenye sherehe za Ballon D'or mnamo Oktoba 30, ambapo alitambuliwa kuwa mchezaji bora chini ya miaka 21.

"Lazima niwe na malengo makubwa, kushinda kura ikiwezekana. Ninafurahia kuichezea nchi yangu, England, na Real Madrid. Shinikizo ni kubwa lakini ninafurahi sana kuwakilisha timu hizi mbili. Nitatia juhudu zote zangu kushinda mataji kwa nchi yangu na kwa Real Madrid."

Bellingham na tuzo

Bellingham amekuwa akimeremeta tangu ajiunge na Madrid kwa kitita cha pauni milioni 115m kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Kiungo huyo anayeiwakilisha England, pia amevunja rekodi iliyokuwa ikishikiliwa na Cristiano Ronaldo, ya mchezaji aliyeifungia Real Madrid mabao mengi katika mechi 15 za kwanza.

Kufikia sasa, Bellingham amefunga mabao 15 katika mashindano yote akiichezea Real Madrid.

Ubingwa wa Bellingham pia umemwezesha kuwa mchezaji wa kwanza wa Real Madrid kutwaa tuzo hiyo aliposhinda kwenye makala ya 21 ya tuzo hizo za Golden Boy.

TRT Afrika na mashirika ya habari