Borussia Dortmund inaelekea mechi ya mkondo wa pili nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ulaya Uefa ikiongoza kwa bao 1-0 huku ikikutana na Paris Saint-Germain mjini Paris, siku ya Jumanne.
Mshindi wa mechi hii atacheza dhidi ya Real Madrid au Bayern Munich ambao walitoka sare 2-2 katika mechi yao ya kwanza ya nusu fainali nchini Ujerumani.
Goli la Niclas Füllkrug nusu fainali ya kwanza liliipa Borussia Dortmund ushindi wa 1-0 dhidi ya Paris Saint-Germain katika mechi ya kwanza ya nusu fainali nyumbani.
Nyota wa PSG Kylian Mbappé ambaye ndiye mfungaji bora wa timu hiyo msimu huu akiwa na magoli 43 katika mashindano yote, bado anasubiri bao lake la kwanza dhidi ya Dortmund.
Mchuano huu utakuwa wake wa mwisho kwenye Ligi ya Mabingwa katika mji mkuu wa Ufaransa akivaa jezi ya Paris Saint-Germain.
Mbappé anaondoka klabu hii majira ya joto baada ya msimu wake wa saba, akitumaini kukamilisha safari yake na PSG kwa kushinda Kombe la Ligi ya Mabingwa, uwanjani Wembley ifikapo Juni 1.
Real Madrid na Bayern nazo zitakutana katika nusu fainali ya pili Jumatano 8 Mei.
Madrid, Iliyothibitishwa kuwa washindi wa ligi ya Uhispania kwa mara ya 36 Jumamosi, haijapoteza mechi ya nyumbani katika Ligi ya Mabingwa tangu kulazwa 3-2 na Chelsea katika robo fainali ya 2021/22.
Dani Carvajal anarudi kutoka marufuku katika kile kinachoweza kuwa nafasi muhimu kutokana na mbinu za Bayern wiki iliyopita.
Kipa Thibaut Courtois naye alirudi mwishoni mwa wiki baada ya kuwa nje tangu Agosti, akitarajiwa kuimarisha lango la Madrid.