Klabu ya Uhispania ya Real Madrid imekanusha madai kuwa, wako kwenye mazungumzo ya kumsaini mshambuliaji wa Ufaransa na klabu ya Paris Saint-Germain Kylian Mbappe mwishoni mwa mkataba wake mnamo Juni 2024 baada ya ripoti za hivi karibuni kuashiria walikuwa kwenye mazungumzo.
"Kwa kuzingatia taarifa iliyotolewa na kuchapishwa hivi karibuni na vyombo mbalimbali vya habari, ambapo kuna uvumi kuhusu madai ya mazungumzo kati ya mchezaji Kylian Mbappe na klabu yetu, Real Madrid inataka kusema kuwa taarifa hizi ni za uongo na kwamba hakuna mazungumzo hayo yamefanyika na mchezaji ambaye ni wa PSG," Madrid ilisema katika taarifa.
Gazeti la uhispania la Marca lilisema alhamisi kwamba Madrid inamtazamia Mbappe kujiunga na klabu hiyo mwaka ujao, huku kikosi kikiamini "atatua Santiago Bernabeu".
Mbappe amekuwa akichumbiwa na Madrid kwa miaka kadhaa lakini alikataa kujiunga na Los Blancos kwa kusaini mkataba mpya na PSG mnamo Mei 2022 licha ya madai mbalimbali kwamba alikuwa amekubali kujiunga na Real Madrid.
Mapema msimu huu, Mbappe alifungiwa na PSG hadi agosti 13 baada ya kukataa kurefusha mkataba wake.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 24, aliachwa nje ya ziara ya klabu ya kabla ya msimu nchini Japan na Korea Kusini na alikosa mechi ya kwanza ya Ligue 1 ya mabingwa wa Ufaransa katika kipindi hicho cha mzozo.
Hatimaye Mbappe alirejeshwa tena kwenye kikosi baada ya kufanya "majadiliano mazuri na yenye manufaa" na klabu hiyo.