Rais wa zamani wa Côte d'Ivoire Henri Konan Bedie amezikwa ziku ya Jumamosi katika kijiji chake, miezi 10 baada ya kifo chake.
Wawakilishi kutoka makabila yote nchini humo walisafiri hadi kijiji cha mashariki cha Pepressou kutoa heshima za mwisho kwa Bedie, ambaye alijulikana sana kwa herufi zake za kwanza za HKB.
Maelfu ya waombolezaji walifurika katika eneo la Pepressou siku ya Jumatatu kwa shughuli hiyo.
Bedie alimrithi baba wa taifa la Côte d'Ivoire Felix Houphouet-Boigny, kama Rais kati ya 1993 hadi1999 – ambapo alipinduliwa na jeshi katika mapinduzi ya kwanza kabisa ndani ya nchi hiyo.
Mazishi yaliyosubiri kwa muda mrefu
Bedie alifariki dunia Agosti 1, 2023 akiwa ndiye kiongozi wa chama kikongwe nchini humo cha Democratic Party.
Maandalizi ya mazishi hayo yamechukua muda mrefu kufuatia mchakato wa kuchagua tarehe ya maziko kwa wanafamilia wake na viongozi wa jadi wa kabila la Baule .
Hadhi yake kama rais wa zamani pia ilirefusha mchakato huo kwani sherehe zilipaswa kutayarishwa katika makao makuu ya PDCI na ikulu ya rais mjini Abidjan ambapo heshima ilitolewa kwake Mei 24.
Mahudhurio katika mazishi ya Pepressou yaliongezeka baada ya mikesha ya Ijumaa, iliyofuatiwa na ibada siku ya Jumamosi.
'Mpenda Amani'
"Licha ya ratiba yake na umri wake, bado angetenga muda wa kutetembelea," amesema Komenan Attou, mkulima wa kijiji cha Pepressou ambaye pia alimsifu kiongozi huyo wa zamani kama "mpenda amani aliyependa kusaidia watu."
Nina Aya Ipou, msusi kutoka kijiji hicho alitokwa na machozi wakati akiwa anamuelezea HKB.
"Alikuwa ni baba yetu, alitufanyia mengi. Nimeishiwa maneno," alisema.
Aliongeza: "Alitujengea nyumba, akatupa ajira. Alinisaidia katika ofisi yangu ."
Nyumba kadhaa zimejengwa
Nyumba nyingi zilijengwa wakati wa utawala wa HKB na kulikuwa na mipango ya makazi ya kiongozi huyo wa zamani.
Ujenzi wa jengo hilo, ambalo sasa limetelekezwa na kumea magugu, ulianza mwaka 1996 lakini ulikatizwa na mapinduzi mwaka 1999.
Akiwa amezaliwa Mei 5, 1934 katika familia ya wakulima wa kakao, HKB pia alikuwa waziri na rais wa Bunge la Kitaifa kabla ya kuwa mkuu wa nchi.