Na Coletta Wanjohi
TRT Afrika, Istanbul, Uturuki
Unapoenda kununua matairi ya gari, ukisema unapendelea yale yanayotoka nchi za kigeni, unajua kuwa mali ghafi ya kutengeza mipira huenda imetoka Afrika?
Kuanzia laptop unayotumia, carpet ulilotandika sebuleni, kiti ambacho umekalia, huenda vyote hivi vimetengenezwa na mipira inayotoka Afrika.
Hii inaonyesha jinsi Afrika inavyochangia katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali duniani.
Ripoti zinaonyesha bara lilizalisha takriban tani milioni 1.5 za mpira au rubber mnamo 2022, sehemu kubwa ya uzalishaji duniani ambayo ilikadiriwa kuwa tani milioni 15.1.
Ivory Coast inaongoza barani Afrika kwa uzalishaji wa zaidi ya tani 600,000 kwa mwaka, ikifuatiwa na Nigeria na Cameroon.
Nchi nyengine zinazozalisha mipira ya asili kwa kiwango kikubwa ni pamoja na Ghana, Liberia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Congo na Guinea. Mipira hutoka katika miti maalumu.
Wakati wa uvunaji wa mpira, dutu kama utomvu wa maziwa inayopatikana kwenye magome ya miti maalumu, hasa mti wa Hevea brasiliensis, unaojulikana pia kama mti wa mpira.
Wataalamu hufanya chale sahihi kwenye gome la mti kwa kutumia chombo maalumu.
Chale hizi zinaruhusu mpira kutiririka nje ya mti.Mchakato huu hurudiwa kwenye miti mingi hadi mpira wa kutosha ukusanywa.
Mara tu mpira unapokusanywa, hupitia mfululizo wa hatua za uchakataji ili kuugeuza kuwa mpira tunaoufahamu.
Takwimu kutoka World Rubber Organisation zinaonyesha kuwa China inaongoza kwa matumizi ya mipira duniani na hivyo kuwa mnunuzi mkubwa huku mwaka 2022 ilitumia tani milioni 5.7 ya mipira.
India inafuata.
Nchi za ulaya zinatumia 30% ya mipira inayozalishwa Afrika. Mingi ya mipira inaenda kwa makampuni ya kimataifa wa kutengenezea matairi ya gari na viungo vingine vya sekta ya usafirishaji.
Na hivyo inavutia makampuni makubwa kimataifa. Makampuni haya yamelaumiwa kwa kuwanyanyasa wakulima wadogo wanaozalisha mipira hii. Kwa mfano, kufikia 2023 kilo moja ya mipira ya asili iliuzwa kwa $1.70.
Baada ya uboreshaji wa mipira hiyo, hata hivyo makampuni makubwa hupata faida nyingi sana huku mkulima anayeshughulikia miti ya raba anabaki katika hali duni.
Makampuni makubwa ya kigeni yamekaumiwa kwa kumiliki ardhi kubwa kwa ajili ya kutosheleza mahitaji yao ya mipira huku wananchi wakikosa kufaidika.
Pia kumekuwa na ripoti kuwa huku mahitaji ya mipira ikiongezeka na makampuni kupanua maeneo ya uzalishaji barani Afrika inaathiri mazingira.
Mahitaji ya mipira yanaongezeka duniani na hii inamaanisha kuwa Afrika ina uwezo wa kuchangia zaidi katika soko la kimataifa.
Swahili ni je, nini kifanyike ili mkulima mdogo ambaye ndiye mzalishaji mpira afaidike ipasavyo?