Tanzania kucheza na Misri mechi ya kirafiki mjini Cairo huku Mo Salah na Mbwana Samatta wakiwa matumaini ya pande hizo. Picha: Reuters

Huku ikiendelea na safari yake ya kujiimarisha kuelekea michuano ya Afcon 2023 Côte d'Ivoire, timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars itapiga mechi ya kirafiki dhidi ya Misri mjini Cairo, leo Jumapili.

Taifa stars, ambayo imetua Cairo mwanzoni mwa mwezi huu wa Januari kuweka kambi ya maandalizi, inazidi kujiandaa ikilenga matokeo bora kwenye hatua ya makundi ambapo imejumuishwa katika kundi F pamoja na Morocco, Zambia, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Kulinga na ratiba rasmi ya michuano yake nchini Côte d'Ivoire, Taifa Stars itafungua kampeni yake ya Afcon kwa mechi inayotabiriwa kuwa ngumu dhidi ya Morocco Januari 17, ikifuatiwa na mchuano dhidi ya 'Chipolopolo' ya Zambia Januari 21 kabla ya kumaliza kazi dhidi ya DR Kongo Januari 24.

Kwa upande wa Misri, mchuano wake dhidi ya Tanzania ndio mechi yake ya mwisho ikiendelea kunoa makali yake kuelekea dimba la AFCON 2023.

Mkufunzi wa Mafarao wa Misri, Mreno Rui Vitoria na kocha mwenza wa Tanzania Adel Amrouche wanatarajiwa kuwatathmini wachezaji wao wote katika kikosi chao wakati wa mechi hiyo ya kirafiki ili kubaini safu ya mwisho kabla ya kuanza kwa mashindano hayo.

Wenyeji Misri wako kundi B, huku wakitarajiwa kuanza kampeni yao ya kusaka taji lao la 8 tarehe 14 Januari dhidi ya Msumbiji kabla ya kukabiliana na Ghana tarehe 18 Januari.

TRT Afrika na mashirika ya habari