Hassan Sheikh Mohamud amehimiza kuheshimiwa kwa mamlaka ya Somalia baada ya Somaliland kutia saini makubaliano yenye mzozo na Ethiopia kwa ajili ya kupata bahari. / Picha: AA

Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alikuwa akizuru Eritrea siku ya Jumatatu - wiki moja tu baada ya eneo lililojitenga la Somaliland kufikia makubaliano na Ethiopia ambayo yameibua mvutano katika Pembe ya Afrika.

Somalia imekataa vikali makubaliano hayo, ambayo yanaipa Ethiopia isiyo na ufuo uwezo wa kutumia Bahari Nyekundu kupitia Somaliland - eneo linalojitenga la Kaskazini Magharibi.

Kuwasili kwa Mohamud mjini Asmara kulitangazwa na ofisi yake na wizara ya habari ya Eritrea katika machapisho tofauti kwenye X, ikiambatana na picha zake akikaribishwa na Rais wa Eritrea Isaias Afwerki.

"Viongozi hao wawili watajadili masuala ya manufaa kwa mataifa yote mawili ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano na kukuza ushirikiano," ofisi ya Mohamud ilisema.

'Uchokozi'

Somalia imeutaja mkataba wa kushtukiza wa makubaliano (MoU) uliotiwa saini Januari 1 mjini Addis Ababa kuwa ni kitendo cha "uchokozi" na ukiukaji wa uhuru wake, na kuomba uungwaji mkono wa kimataifa.

Umoja wa Afrika na Marekani miongoni mwa nchi nyingine zimetoa wito wa utulivu na heshima kwa uhuru na uadilifu wa ardhi ya Somalia.

Somaliland, nchi ambayo ilikuwa chini ya ulinzi wa Uingereza, ilitangaza uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991 lakini hatua hiyo haijatambuliwa kimataifa na inapingwa vikali na serikali kuu ya Mogadishu.

Mkataba wa Januari 1 uliipa Ethiopia fursa ya kupata huduma za kibiashara za baharini na kambi ya kijeshi, huku Somaliland ikiikodisha kilomita 20 za ukanda wa pwani kwa miaka 50.

Ethiopia, nchi ya pili kwa idadi kubwa ya watu barani Afrika na mojawapo ya mataifa makubwa zaidi yasiyo na bahari duniani, ilitengwa na pwani baada ya Eritrea kujitenga na kujitangazia uhuru mwaka 1993 kufuatia vita vya miongo mitatu.

TRT Afrika