Rais wa DRC  - Ikulu ya DRC

Siku ya Ijumaa Septemba 1, rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo , Félix Tshisekedi, ameelezea kusikitishwa na kifo cha watu wapatao arobaini Jumatano Agosti 30 huko Goma katika eneo la Kivu Kaskazini.

Takriban watu 43 waliuawa na wengine 56 kujeruhiwa katika maandamano dhidi ya Umoja wa Mataifa wiki hii Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, serikali ilitangaza Alhamisi.

Makundi ya haki za binadamu yamelaumu jeshi kwa kufyatua risasi wakiwalenga raia.

Kulingana na msemaji wa serikali Patrick Muyaya, Félix Tshisekedi alitoa maoni yake wakati wa mkutano wa baraza la mawaziri Ijumaa.

Muyaya anaripoti kuwa mkuu huyo wa nchi aliwataka naibu mawaziri wakuu wa mambo ya ndani ya nchi, Ulinzi na Sheria “kutoa taarifa kwake haraka iwezekanavyo kuhusu mazingira yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 43, ili vikwazo vikali vichukuliwe dhidi ya waliohusika na tukio hili la kusikitisha."

Vurugu za ukandamizaji wa maandamano yaliyoandaliwa na dhehebu la 'wazalendo' ziligeuka kuwa mauaji siku ya Jumatano wakati vyombo vya sheria na utulivu vilipovunja maandamano hayo yaliyokuwa yamepigwa marufuku na mamlaka ya mkoa.

Idadi rasmi ya waliofariki ni 43 na 56 kujeruhiwa.

Takriban waandamanaji mia moja walikamatwa, akiwemo kiongozi wa dhehebu hilo, Ephraïm Bisimwa.

Kesi yao katika flagrante ilianza Ijumaa 1 Septemba katika uwanja wa Unité huko Goma.

Waandamanaji hao walikuwa wakielezea kukerwa kwao na uwepo wa MONUSCO, vikosi vya jumuiya ya Afrika Mashariki na mashirika ya kimataifa huko Kivu Kaskazini.

Vyanzo vya mahakama vinaripoti kuwa uchunguzi unaendelea kujua ni nani alihusika na mauaji hayo.

Matukio haya ya vurugu ni sehemu ya mfululizo wa mashambulizi na maandamano dhidi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, unaoshutumiwa kwa kutofanya kazi katika vita dhidi ya makundi yenye silaha.

Mnamo Julai 2022, katika miji kadhaa katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini, waandamanaji walivamia vituo vya Monusco.

Kulingana na mamlaka, watu 36, ikiwa ni pamoja na askari wanne wa kulinda amani, waliuawa.

TRT Afrika