ziara hii unatarajiwa kutangaza fursa za biashara na uwekezaji za Tanzania ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka India./ Picha : Ikulu Tanzania 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewasili leo Mjini Delhi India kufuatia mualiko wa mwenzake wa India Mhe. Droupadi Murmu.

Ziara hii ya siku nne inatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katik anyanja mbali mbali ikiwemo sekta za kimkakati kama vile afyta, sekta ya viwanda na biashara, sekta ya ulinzi na usalama, elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, uchumi wa buluu, maji, na kilimo.

Pia ziara hii unatarajiwa kutangaza fursa za biashara na uwekezaji za Tanzania ili kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara kutoka India.

India ni mdau mkubwa wa maendeleo Tanzania ambapo hadi sasa India inachukua nafasi ya 5 kwa kiwango cha uwekezaji Tanzania.

Kwa mujibu wa ikulu ya Tanzania kupitia mtandao wake wa X, zamani Twitter, Ongezeko la biashara kati ya Tanzania na India inakadiriwa kufikia dola za Kimarekani bilioni 3.14 mwaka 2022 ukilinganisha na Dola za Kimarekani bilioni 2.14 mwaka 2017.

Uhusiano wa muda mrefu

Rais Samia alipokewa kwa mbwembwe alipowasili uwanja wa ndege wa Kimataifa wa wa Indira Gandhi, New Delhi nchini India.

Zaidi ya miradi 630 ya Uwekezaji imesajiliwa kutoka India ndani ya Tanzania kati ya mwaka 2021 -2022 /Picha : Ikulu Tanzania

Hii ni ziara ya kwanza kwa kiongozi wa kitaifa wa Tanzania kutembelea India tangu 2015.

Kwa upande wa India, mara ya mwisho ya ziara kama hii ya kiongozi wa kitaifa kuja Tanzania ni mwaka 2016, alipozuru Narendra Modi, Waziri mkuu wa Jamhuri ya India.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na India ulianza tangu mwaka 1961. India ilifungua Ubalozi wake mwaka 1961 na Tanzania ilifungua Ubalozi wake nchini India mwaka 1962

Miongoni mwa miradi mikubwa iliyowekezwa na India ndani ya Tanzania ni katika sekta ya maji, ambapo miradi imetekelezwa kwa ushirikiano na serikali ya India.

Mfano nimradi wa Tabora-Igunga-Nzega wa takriban shilingi Bilioni 617 za Tanzania ambao umekamilika, pamoja na miradi mingine katika miji 28 kwa gharama ya Shilingi Trilioni 1.48 ambayo bado inaendelea na ujenzi.

Zaidi ya miradi 630 ya Uwekezaji imesajiliwa kutoka India ndani ya Tanzania kati ya mwaka 2021 -2022 kwa thamani ya takriban dola Bilioni 3.74 za Marekani.

TRT Afrika