Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa hatua za dharura kuchukuliwa kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi.
''Kuna hatari kubwa, na hatua inapaswa kuchukuliwa sio kesho bali leo na haswa sasa,'' amesema Rais Samia alipohutubia kongamano la Mabadiliko ya Tabia Nchi lililofanyika jijini Nairobi.
Rais alisema kuwa hali ilipofikia, Waafrika hawana budi kunyakua fursa iliyopo na kujiweka mbele katika kutoa suluhisho za ukuzaji wa nishati ya kijani na njia za kumaliza gesi ya kaboni kwenye mazingira.
''Hii itasaidia katika kuimarisha jamii zetu na uchumi wetu,'' aliongeza Rais.
Rais Samia alisisitiza kuwa, japo bara la Afrika lina mchango mdogo katika uchafuzi wa mazingira, wao ndio wanaopata athari kubwa zaidi ya mabadiliko ya Tabia Nchi kwa kuwa ndilo bara lenye siri ya suluhu kwa tatizo hilo.
Utajiri wetu haki yetu
Akizungumzia ripoti ya Maendeleo ya Uchumi iliyotolewa hivi karibuni, Rais Samia alisema inaonyesha uwezekano wa Afrika kukamata minyororo ya ugavi wa teknolojia ya kimataifa na alisisitiza umuhimu wa kuunda hiyo kwa maendeleo ya Afrika na kuzingatia mabadiliko ya Tabia Nchi.
Kongamano hilo la mabadiliko ya Tabia Nchi lilihudhuriwa na zaidi ya wajumbe 30,000 wakiwemo marais, viongozi wa mashirika ya kimataifa na wadau wa Mazingira.
Wengi waliozungumzia nguvu ya Bara la Afrika, walitaja utajiri wake kama vile madini muhimu. Rais Samia alisema basi madini muhimu yanapaswa kutoa michango muhimu katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na fursa za ajira.
''Afrika inapaswa kukaa imara katika kutumia nyenzo zetu kwa maendeleo yetu,'' alisema.
Kongamano hili linatangulia mkutano wa kimataifa wa Cop28, unaoangazia ukataji wa gesi za kaboni na uhifadhi wa mazingira, utakaofanyika kaitika falme za kiarabu UAE.