Rais wa Senegal Macky Sall alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi wa Urais mnamo Februari 3.

Rais wa Senegal Macky Sall ameahidi Ijumaa kuandaa uchaguzi wa urais "haraka iwezekanavyo" baada ya baraza la Katiba kupuuza uamuzi wake wa kuahirisha uchaguzi wa mwezi huu.

"Rais wa Jamhuri anatarajia kutekeleza kikamilifu uamuzi wa Baraza la Katiba," rais alisema katika taarifa.

Tangazo hilo limefika muda mfupi baada ya kundi kuu la kikanda la Afrika Magharibi ECOWAS kutoa wito kwa mamlaka nchini Senegal kupanga tarehe mpya ya uchaguzi wa Urais kwa mujibu wa uamuzi wa Baraza la Katiba.

Zimesalia siku 10 tu kabla ya tarehe iliyopangwa awali ya uchaguzi, Februari 25 na wagombea wengi hawajafanya kampeni tangu Sall alipotoa amri yake Februari 3, saa chache kabla ya kampeni kuanza rasmi.

Ilidhaniwa kwamba upinzani wowote kutoka kwa rais wa kupinga uamuzi wa Baraza la Katiba juu ya uchaguzi ulioahirishwa ungezua machafuko zaidi. Mgogoro wa uchaguzi wa wiki nzima tayari umesababisha maandamano ya vurugu na maonyo ya utawala wa kimabavu.

AFP