Rais wa Kenya, William Ruto, ameelezea maandamano ya Jumanne ambayo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua watano na kujeruhi zaidi ya 90 kama "ya uhaini."
Katika hotuba kwa taifa Jumanne usiku, Ruto alisema serikali itachukulia hatua wapangaji, wafadhili, waongozaji, na washiriki wa vurugu na machafuko.
Wakenya kutoka sehemu mbalimbali za nchi, ikiwa ni pamoja na mji mkuu Nairobi, walipambana na polisi kwa sehemu kubwa ya siku, wakipinga kodi wanazozitaja kuwa "nzito" na "zisizo za kibinadamu."
Rais Ruto anapanga kutoza kodi zaidi kwa taulo za usafi zinazoagizwa kutoka nje, simu za mkononi na pikipiki, pamoja na kutoza kodi kwa ardhi inayouzwa chini ya mipango ya amana ya familia.
Ruto, ambaye amepanga bajeti ya juu kabisa ya shilingi trilioni 3.9 – au dola bilioni 30 za kimarekani – kwa mwaka wa fedha 2024/2025, anasema Kenya inahitaji mapato zaidi ili kuepuka kutegemea mikopo kupita kiasi.
Ili kudhibiti maandamano, serikali Jumanne ilipeleka jeshi kusaidia polisi katika operesheni hiyo.