Rais mpya wa Ghana John Mahama ameamuru kurejeshwa kwa pasipoti za kidiplomasia zilizotolewa na utawala uliopita kwa mawaziri wa zamani, wabunge na wenzi wao kama sehemu ya juhudi za kuimarisha uadilifu wa hati za kusafiria.
Agizo hilo pia linaathiri hati za kusafiria za kidiplomasia zilizotolewa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita kwa majaji wa zamani, mabalozi, viongozi wa kimila na wafanyabiashara.
Rais aliweka makataa ya Januari 24 kwa pasipoti hizo kurejeshwa kwa wizara ya maswala ya kigeni.
Agizo hilo "linalenga kuzuia matumizi mabaya" ya pasipoti za kidiplomasia na pasipoti za huduma, wizara ya mambo ya nje ilisema katika taarifa.
Ilisema pasipoti zilizorejeshwa zitakaguliwa ili kuhakikisha zinakidhi vigezo vya kustahiki kutolewa.
Mgogoro wa kiuchumi
Rais Mahama aliapishwa siku ya Jumanne na kuahidi kuirejesha kampuni inayozalisha dhahabu na kakao ya Afrika Magharibi na kuiondoa katika mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kutokea kwa miongo kadhaa.
Mahama alipata asilimia 56 ya kura katika uchaguzi wa rais wa taifa hilo uliofanyika Desemba 9, na kuwashinda mgombea wa chama tawala na Makamu wa Rais Mahamudu Bawumia, aliyepata asilimia 41.
Anachukua nafasi kutoka kwa rais anayeondoka Nana Akufo-Addo, ambaye alihudumu kwa mihula miwili madarakani.
Nchi hiyo yenye watu milioni 33 ndiyo inayoongoza kwa mauzo ya dhahabu barani Afrika na ya pili duniani kwa uzalishaji wa kakao.