Rais wa Senegal Macky Sall siku ya Ijumaa alisema kuwa atatii kikamilifu uamuzi wa mahakama uliobatilisha kuahirishwa kwa uchaguzi wa urais hadi Desemba, na kuahidi kufanya mashauriano kuandaa kura hiyo haraka iwezekanavyo.
Sall "amezingatia" uamuzi wa baraza hilo na ombi la uchaguzi ufanyike haraka iwezekanavyo, ofisi ya rais ilisema katika taarifa yake Ijumaa.
"Rais ananuia kutekeleza kikamilifu uamuzi wa baraza la katiba," iliongeza.
Sall amekuwa chini ya shinikizo kubwa kukubali uamuzi huo. Mgogoro wa wiki nzima wa uchaguzi tayari umesababisha maandamano ya vurugu na maonyo ya unyanyasaji wa kimabavu katika mojawapo ya demokrasia imara zaidi ya Afrika Magharibi iliyokumbwa na mapinduzi.
Mswada ambao ulirudisha nyuma uchaguzi wa Februari 25 na kuitumbukiza nchi katika sintofahamu ya uchaguzi ulibatilishwa siku ya Alhamisi na Baraza la Katiba la Senegal.
Maandamano mengine ya kupinga ucheleweshaji huo yalipaswa kuanza katika mji mkuu wa Dakar wakati tu ofisi ya rais ilitoa majibu ya Sall. Takriban watu mia moja walijitokeza huku polisi wakizuia ufikiaji wa vituo vya mikutano na kurusha vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji.
Mkazi wa Dakar, Mohamed Alpha Diop alikaribisha matarajio ya kucheleweshwa kwa muda mfupi kwa uchaguzi. "Nadhani itatuliza mambo," alisema.
Sall alisema awali alichelewesha uchaguzi kutokana na mzozo wa orodha ya wagombea na madai ya rushwa ndani ya Baraza la Katiba alioonya kuwa itadhoofisha uaminifu wa uchaguzi huo. Baraza hilo limekanusha tuhuma hizo.
Wadau wengi wa upinzani wamekaribisha uamuzi wa baraza hilo na wengine wamemtaka Sall kupanga tarehe ya uchaguzi kabla ya Aprili 2, wakati mamlaka yake yatakapokamilika.
"Tarehe 2 Aprili, rais ataondoka," alisema kiongozi wa upinzani Khalifa Sall, ambaye amelaani matukio ya hivi karibuni kama "mapinduzi ya taasisi".
"Sasa hali zinahitaji kubadilishwa, kwa sababu kufanya uchaguzi Februari 25 hakutawezekana," alisema wakati wa mahojiano huko Dakar, akiongeza kuwa alikuwa tayari kushiriki katika mazungumzo na pande zote ili kukubaliana juu ya tarehe mpya.