Kufuatia vita vinavyoendelea nchini Sudan tangu Aprili 15, 2023, wahamiaji wa Ethiopia wanaoishi humo pamoja na wakimbizi wa Ethiopia waliosajiliwa Sudan wamelazimika kurudi nchini mwao.
Kufikia Agosti 7, 2024 Shirika la Kimataifa la Uhamiaji la IOM, limerekodi Waethiopia 57,568 waliovuka mpaka. Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi, UNHCR lilitambua watu 11,771 waliosajiliwa hapo awali nchini Sudan kama wakimbizi waliorejea Ethiopia.
Sudan, ambayo ina rekodi ya muda mrefu ya kuwapa makazi wakimbizi kwa ukarimu, iliwahi kuwa makazi ya zaidi ya wakimbizi milioni 1.
Sudan ilikuwa nchi ya pili kwa idadi kubwa ya wakimbizi barani Afrika - haswa kutoka Sudan Kusini, Eritrea, Syria, na Ethiopia, na pia Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad na Yemen.
Maelfu ya wananchi kutoka hasa kaskazini mwa Ethiopia walikimbilia nchi jirani ya Sudan kuanzia Novemba 2020. Hii ilikuwa baada ya vita kuzuka kati ya jeshi la taifa la Ethioipia na vikosi vilivyounga mkono chama cha Tigray people Liebrataion Front, TPLF.
Ilikuwa mvutano wa kisiasa ambao ulidumu hadi Novemba 2022 wakati pande zote mbili zilipotia saini makubaliano ya amani ya kusitisha vita.
Na sasa Sudan kukiwa hakukaliki kutokana na vita nchini humo, waliokimbilia Sudan sasa wanalazimika kutafuta afueni tena walikotoroka.