Patrick Wanjohi
Nairobi, Kenya
Ukiingia katika nyumba ya Rachel Kabue paka wa kimo, rangi na miundo tofauti wanakukaribisha.
Kama hujawahi kuona paka wengi wakiwa sehemu moja na kwa wakati mmoja, basi taswira iliyopo nyumbani kwa Rachael itakustaajabisha.
"Tuna paka 635," Rachel anaiambia TRT Afrika huku akimkumbatia na kumpapasa paka anayerukaruka mikononi mwake.
"Idadi ya paka imepungua kidogo kwa sasa kwa sababu tumekuwa tukiwatoa baadhi kwa ajili ya kuasiliwa," anaongeza.
Mnamo 2013, Rachael mwenye miaka 51, ambaye watu humuita "Mama wa Paka Kenya," alianza kazi yake ya kuwasaidia na kuwaokoa paka walio katika mazingira magumu.
Safari yake ilianza na paka mmoja ambae alimuokota baada ya kutelekezwa. Baada ya hapo, akajipata anaendelea kukusanya zaidi kila siku.
Amekusanya paka waliotelekezwa mitaani na wengine, anasema huwapata wakiwa milangoni kwake.
Mama huyo wa watoto watano sasa anaendesha hifadhi anayoita Nairobi Feline Sanctuary katika eneo la Utawala, ambalo ni kilomita 20 kutoka jijini Nairobi.
Paka wengi kati ya 635 wanahifadhiwa katika uzio wa mbao uliopakwa rangi nyeupe. Unaingiza hewa ya kutosha katika ua wa mbele ya nyumba.
Paka waliobaki wanafugwa katika eneo alilolitenga kama kliniki ndani ya nyumba.
Rachel na familia yake, awali walikuwa waliishi katika nyumba hiyo ya vyumba vitatu kabla ya kuhama, ili kutoa nafasi ya kutosha kwa paka hao. Eneo hilo sasa hivi ndio limepewa jina la Nairobi Feline Sanctuary.
Katika eneo hilo, siku inapoanza kunakuwa na shughuli mbalimbali kwa wafanyakazi. Wengine kazi yao mahususi kufanya usafi, huku wengine wakiandaa chakula kwa ajili ya wanyama hao.
Paka hawa hulishwa mara mbili kwa siku. Chakula wanachopenda zaidi ni kuku. Na kila wiki, wanakula zaidi ya kilo 12 za kuku.
"Wanapenda kuku sana, siku ambazo wamekula kuku tunajaribu kuwapa chakula mchana kwa sababu kila mara wanahisi kama hawajala," Rachel anaelezea.
Rachel ana shughuli nyingi sana. Anapokea simu kutoka kwa watu mbalimbali wanaopenda kufuga paka kila baada ya dakika chache huku wengine wakipiga simu kumpa baadhi ya paka yao.
Kila baada ya siku kumi na nne baada ya kuokolewa, Rachel humpa kila paka jina linalolingana na hali au tabia yake.
Tukiwa hapo tunamsikia Konde na Chai, wakiitwa mara kwa mara. Anasema ana uhusiano maalum na kila paka anayemtaja.
Ananionyesha makovu yaliyoachwa na mikwaruzo mingi ambayo yamesababishwa na paka hao, haswa mikononi.
Mikwaruzo hiyo, anasema, haimsumbui kwa sababu paka hutumia mikwaruzo kama sehemu ya mawasiliano pindi wanapokuwa katika hali fulani au wanapohitaji kitu.
Rachel anakubali kwamba, kuwalisha na kuwaandalia mahitaji yao ya matibabu ni ghali, na yeye hutegemea hasa akiba yake binafsi na watu wanaomtakia mema kumsaidia kulipia gharama hizo.
Ufugaji pia ni mgumu sana katika idadi hii ya watu, na kwa kuwa paka kawaida huzaa watoto watatu hadi sita mara moja, idadi inavyozidi kuwa kubwa, ndivyo anavyozidi kupata changamoto ya kuwatunza.
Katika hifadhi hii, paka wa kike na wa kiume wanafanyiwa mpango wa uzazi, kwa usaidizi wa madaktari wa mifugo ili kudhibiti idadi.
"Tunapata paka ambao huja wakiwa wajawazito, na tunawaacha wajifungue, wanyonyeshe kwa wiki 8 na kisha tunawafunga uzazi kupitia usaidizi wa madaktari," Rachel anaeleza.
Wataendelea kuja
Rachel anasema familia yake, haswa watoto wake, wanaunga mkono juhudi zake na hata kumsaidia kuwaokoa baadhi ya paka.
Katika mahojiano yake na TRT Afrika, Rachael, anasema tatizo lake kubwa ni uhaba wa eneo la kutosha kuwaweka paka wote.
"Hivi majuzi tulipata ardhi kando ya Ziwa Victoria, (kilomita 354 kutoka Nairobi) na tumeanza kujenga makazi mapya huko," anaiambia TRT Afrika, "Ardhi ni kubwa, haitakuwa ni makazi ya paka pekee, tutawaokoa wanyama wengine pia."