Maiti tiza zilipatikana, saba za wawanawake na mbili za wanaume, mamlaka ya IPOA imesema / Picha : Reuters 

Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) imetaka uchunguzi wa kisayansi ufanyike haraka kuhusu miili tisa iliyogunduliwa kwenye machimbo ya mawe eneo bunge la Embakasi Kusini, jijini Nairobi.

Mwenyekiti wa IPOA Anne Makori alisema shirika hilo lilituma timu ya dharura "ili kupata taarifa zote ambazo zinaweza kuwa muhimu katika kufichua mazingira. yanayohusiana na vifo hivyo”.

Katika taarifa aliochapisha mtandaoni. mwenyekiti Anne Makori alisema kuwa kati ya maiti hizo tisa, saba zinaaminiwa kuwa za wanawake na wanaume wawili na zilikuwa katika hali ya kutamausha.

''Miili hiyo iliyotiwa kwenye mifuko ya plastiki na kufungwa kwa kamba za nailoni ilikuwa na alama za kuteswa na kukatwakatwa,'' alisema Makori.

Maiti hizo zilikutwa chini ya mita mia moja kutoka kituo cha polisi na kuzua tetesi kwamba huenda polisi walihusika.

IPOA inasisitiaza kuwa uchunguzi kamili utafanywa na hatua kamili ya kisheria kuchukuliwa kwa waliohusika, hata wakiwa polisi.

''Ukweli kutokana na uchunguzi utaamua hatua itakayofuata. Mamlaka haitasita kutoa mapendekezo ikiwa ni pamoja na lakini bila ukomo wa kushitakiwa wote watakaokutwa n ahatia,'' ilisema taarifa hiyo ya IPOA.

Mkuu wa Polisi ajiuzulu

Haya yanakuja wakati Mkuu wa polisi nchini Kenya, Japheth Koome, amejiuzulu huku kukiwa na ukosoaji kuhusu jinsi polisi walikabiliana na maandamano ya hivi majuzi dhidi ya serikali yaliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 30.

Katika taarifa, Rais William Ruto alitangaza kukubali kujiuzulu kwa Koome kama Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi na kumteua naibu wake, Douglas Kanja, kukaimu mara moja.

Siku moja kabla, Rais Ruto aliwatimua mawaziri wake wote.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na waangalizi wanaoungwa mkono na serikali, wameshutumu polisi kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji, ikiwa ni pamoja na kufyatua risasi za moto kwenye umati wa watu. Awali Ruto alisema uchunguzi utafanywa kubaini kosa la polisi kwa vifo hivyo.

Katika taarifa yao mtandaoni, IPOA ilichapisha vipengee nane vya sheria inyoelezea upana wa nguvu ya polisi na hatua za kuchukuliwa kutokana na uvunjifu wa sheria yoyote inayohusika kutokana namatendo ya polisi.

Masharti ya kufuatwa na polisi

Miongoni mwa masharti yaliyotajwa ni pamoja na kuwa polisi lazima wajitambulishe wanapotekeleza sheria, lazima waepuke kutumia nguvu hadi pale inawalazimu na kuwa ni wajibu wa polisi kutoa huduma ya matibabu kwa yeyote atakayejeruhiwa kutokana na hatua zao.

Pia katika orodha hiyo, IPOA imesema kuwa ni wajibu wa polisi mhusika kuripoti maafa yoyote au majeruhi aliyosababisha kutokana na hatua aloyochukua, na kukosa kuripoti kwa IPOA ni kosa litakaloadhibiwa.

''Kufuata amri ya mkubwa'' sio sababu halali ya kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia,'' IPOA imesema.

TRT Afrika