Hali ya kawaida ilikuwa inarejea polepole katika maeneo yanayozunguka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Haiti katika mji mkuu Port Au Prince'/ Picha : X- National Police Service Kenya 

Ujumbe wa Kimataifa wa Msaada wa Usalama (MSS) unaoongozwa na Kenya nchini Haiti umezidisha shughuli za pamoja katika juhudi za kurejesha hali ya kawaida katika eneo linalodhibitiwa na magenge katika taifa la Karibea.

Wanachama kadhaa wanaohusika na magenge wametiwa nguvuni katika maeneo ya Ganthier na Delmas, katika mji mkuu Port au Prince.

Kurugenzi ya mawasiliano ya Polisi Kenya, NPS ilisema kuwa oparesheni hizo zimesababisha kukamatwa kwa wanachama kadhaa wa genge.

''Doria hizi za pamoja na operesheni zimesababisha kukamatwa kwa wanachama kadhaa wa magenge na kurejea katika hali ya kawaida katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa yametawaliwa na magenge,'' ilisema taarifa ya polisi.

Taarifa hiyo ya polisi ilifichua kuwa kikosi cha mapema cha maafisa kutoka Jumuiya ya Karibea (CARICOM) kiliwasili Haiti chini ya Kamandi ya Kanali Kevron Henry kutoka Jamaika mnamo Septemba 12.

Awali, Kenya ilifichua kwamba hali ya kawaida ilikuwa inarejea polepole katika maeneo yanayozunguka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Haiti katika mji mkuu Port Au Prince, miezi mitatu baada ya kuanza kwa operesheni ya poamoja inayoongozwa na kikosi cha Kenya.

Hata hivyo mwanzoni mwa mwezi Septemba, baada ya ziara yake nchini Haiti, waziri wa mambo ya Nje wa Marekani Anthoiny Blinken alielezea nia ya kuhamisha oparesheni hiyo ya usalama kutoka kwa kikosi huru kinachoongozwa na Kenya na kukabidhiwa na Umoja wa Mataifa chini ya misheni maalum.

Lakini hili linasubiriwa kujadiliwa na kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo kwa sasa linatashwishi kutokana na kuwa Haiti iliwatimuwa kikosi cha Umoja huo kilichokuwepo mwanzoni kufuatia madai ya unyanyasaji wa kingono, udhalilishaji na hata madai ya kusambaza ugonjwa wa kipindupindu, yote yanayodaiwa kufanywa na wanajeshi wa kikosi hicho.

Haiti imekuwa ikikabiliana na kuongezeka kwa ghasia tangu kuuawa kwa Rais Jovenel Moïse mnamo Julai 2021 katika makazi yake ya kibinafsi katika mji mkuu, Port-au-Prince, na kusababisha wito wa kuingilia kati usalama.

Magenge ya kihalifu yameteka miji kadhaa na kuendeleza biashara haramu, ulanguzi wa dawa za kulevya, ubakaji, utekaji na mauaji ya raia kiholela.

TRT Afrika