Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Douglas Kanja Kirocho amesema mauaji nchini humo yameongezeka/Picha. Polisi Kenya

Huduma ya Kitaifa ya Polisi nchini Kenya inasema kuna mtindo wa kuongezeka kwa mauaji nchini humo.

"Uchambuzi linganishi wa kesi za mauaji zilizoripotiwa kuanzia Agosti hadi Oktoba 2022 mpaka 2024 unaonyesha ongezeko kidogo," imesema taarifa ya Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi, Douglas Kanja Kirocho katika akaunti ya X.

Hali hii imezua hofu kwa wananchi huku miili ikipatikana imetupwa.

"Mwaka wa 2024 jumla ya mauaji 339 yamerekodiwa, ikilinganishwa na 336 iliyoripotiwa mwaka 2023 na 341 mwaka 2022," ameongezea.

Kwa sasa Inspekta Jenerali Mkuu anasema uchunguzi wa vifo kadhaa ambavyo kwa jumla zimezua mjadala kati ya raia unaendela.

Willis Anyango Oyieko mwenye umri wa miaka 52 ambaye mwili wake ulianza kuoza, ulipatikana katika mto huko Mugewere katika kaunti ndogo ya Khuisero.

Mwili unaoshukiwa kuwa wa mkazi wa kaunti ya Wajir aliyepotea September 13, 2024, Makadara Nairobi. Mwili wake ulipatikana ukielea katika mto Yahud katika kaunti ndogo ya Wajir Mashariki.

Katika kaunti ya Kajiado James Nyaata Onchiri mwenye miaka 62 na wakili katika kaunti hiyo alionekana mara ya mwisho na msaidizi wake Oktoba 21, 2024 mwendo wa jioni na mwili wake kupatika siku inayofuatia. Camera za CCTV zimemuonyesha msaidizi wake akimvuta kutoka kwenye baa, kumgonga kwa gari na kutoweka.

Katika mji mkuu wa Nairobi wanawake watatu wenye asili ya Kisomali walipatikana wameuawa Oktoba 22, 2024, huku mmoja wao akiwa amekatwa mkono.

Mwili wa Seth Njeri Nyakio mwenye umri ya miaka 23 ulipatikana katika nyumba ya rafiki yake Oktoba 14, 2024 katika mji wa Thika. Uchunguzi wa seriklai umeonyesha alikufa baada ya kunyongwa.

Victoria Mumbua dereva wa teksi katika kaunti ya Mombasa aliripotiwa kupotea Septemba 28, 2024. Polisi katika kaunti ya Nakuru walimnasa mtu na gari yake ambaye alikiri kuwa alimuuwa na kuiba gari yake na kuutupa mwili wake katika barabara ya Mai Mahiu - Naivasha. Mwili wake ulipatikana siku hiyo hiyo, Septemba 28, 2024.

Mauaji ya wanawake

Mwezi Julai 2024 polisi ilimkamata Collins Jumaisi kwa mauaji ya wanawake ambao miili yao ilipatikana eneo la taka la Kware katika mitaa ya Mabanda ya Mukuru, Nairobi.

"Mshukiwa alikiri kuwashawishi, na kuwauwa wanawake 42 tangu 2022, na mauaji ya ya hivi karibuni zaidi yalikuwa ni ya Julai 11. Mshukiwa alidai muathiriwa wake wa kwanza alikuwa mke wake ambaye alimnyonga hadi kufa kabla ya kuukata mwili wake," Mkuu wa Kitengo cha Makosa ya Jinai, Mohamed Amin alisema Jumatatu.

Hata hivyo, mshukiwa alikana mashtaka hayo mahakamani.

Agosti 2024 kwa njia isiyoeleweka mshukiwa alitoroka kizuizini pamoja na wafungwa wengine 12 waliokuwa katika Kituo cha Polisi cha Gigiri, jijini Nairobi.

TRT Afrika