Polisi nchini Kenya wameweka tangazo la kuomba msaada kutoka kwa wananchi la kumkamata Collins Juamisi mshukiwa mshukiwa wa ambaye alitoroka rumande katika kituo cha polisi, Nairobi Agosti 12, 2024.
Katika tangazo la Alhamisi, Agosti 22, 2024, polisi imeahidi kutoa zawadi kubwa ya pesa kwa yeyote aliye na taarifa za kuaminika zitakazopelekea kukamatwa kwa Collins Jumaisi.
"Zawadi kubwa ya pesa taslimu itatolewa kwa mtu yeyote mwenye taarifa za kuaminika zitakazopelekea kukamatwa kwa mshukiwa," taarifa ya DCI imesema.
DCI alitaja kuwa Jumaisi alipangiwa kushtakiwa kwa mauaji lakini akatoroka mikononi mwa polisi wa Gigiri mnamo Jumatatu, Agosti 20, 2024, pamoja na washukiwa wengine 12.
Wengine 12 waliotoroka kizuizini walikuwa raia wa Eritrea.
Maafisa wa polisi wafikishwa mahakamani
Maafisa watano wa polisi wa Kenya walio katika Kituo cha Gigiri, Nairobi walifikishwa Jumatano katika mahakama ya eneo hilo kwa tuhuma za kusaidia kutoroka kwa mshukiwa wa mauaji Collins Jumaisi na wafungwa wengine 12 mapema Jumanne.
Upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali James Gachoka, uliiomba mahakama kuwazuilia washukiwa hao kwa siku 14 huku uchunguzi ukiendelea kuhusu jinsi baadhi yao wanavyodaiwa kusaidia kutoroka kwa Jumaisi na wafungwa wengine 12.
Gachoka alimweleza Hakimu Martha Naanzushi kwamba wamepata picha za CCTV, ambazo kwa sasa zinafanyiwa uchunguzi wa kitaalamu.
Kanda hiyo inadaiwa kuwaonyesha maafisa waliokuwa zamu wakiwasaidia wafungwa kutoroka.
Mkuu wa Polisi wa Kitaifa wa Kenya Gilbert Masengeli aliwaambia waandishi wa habari jijini Nairobi, "Uchunguzi wetu wa awali unaonyesha kuwa utorokaji ulisaidiwa na watu wa ndani."
Maafisa hao, ambao utambulisho wao haujafichuliwa, wanatuhumiwa kwa kuzembea kazini na kusaidia kutoroka kwa wafungwa, miongoni mwa makosa mengine.
Upande wa mashtaka unadai kwamba vitendo vyao vilichangia kutoroka kwa watuhumiwa hao.
Upande wa mashtaka unakuja huku mamlaka ikizidisha msako wa Jumaisi, ambaye anatuhumiwa kwa mauaji ya kikatili na kuwakatakata wanawake 40 na wengine waliotoroka.
Jumaisi, anayejulikana kwa mauaji ya Mukuru, ambapo miili ya waathirika ilipatikana katika machimbo yaliyojazwa maji katika mtaa wa Embakasi, Nairobi, alikosa kufikishwa mahakamani Ijumaa iliyopita.
Hii imezidisha hasira ya umma na kuibua wasiwasi juu ya ufanisi wa mifumo ya haki na usalama.
Urahisi wa kutoroka Kituo cha Polisi cha Gigiri, ambacho kinajulikana kwa ulinzi wa hali ya juu kutokana na ukaribu wake na balozi kadhaa, kumezua uvumi kuhusu uwezekano wa ukiukaji wa usalama au kula njama.