Polisi nchini Kenya wamekana kuhusika katika utekaji nyara wa watu.
Kauli hii, inafuatia mjadala unaoendelea nchini humo ambapo wananchi wakiwalaumu polisi kwa utekaji nyara wa watu waliomkejeli Rais William Ruto kwa njia tofauti.
"Kwa kuepusha shaka Huduma ya Polisi ya Taifa haihusiki na utekaji nyara wowote na hakuna kituo cha polisi kinachowashikilia watu waliotekwa nyara," Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja Kibocho, amesema katika taarifa.
Siku ya Jumatano jioni, mchoraji katuni Kibet Bull na kaka yake waliripotiwa kutoweka, huku ripoti zikisema walitekwa nyara.
Familia za Bernard Kavuli, Peter Muteti na Billy Mwangi wamesema watatu hao walitoweka na picha zao zilizochukuliwa kwa nguvu zilionekana kwenye majukwaa ya vyombo vya habari.
Vijana hao walitoa machapisho yanayodaiwa kuwa na utata yanayomuangazia Rais Ruto kwenye mitandao ya kijamii.
Mnamo Jumatano, Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) imesema imepokea ripoti za utekaji nyara unaodaiwa kutekelezwa na polisi.
Kulingana na IPOA, imepokea ripoti za kutekwa nyara kwa watu 5 kutoka Kajiado, Nairobi na Embu.
“Kwa kuzingatia masharti ya Kifungu cha 6(a) cha Sheria ya IPOA, kinachoitaka Mamlaka kuchunguza malalamiko yoyote yanayohusiana na makosa ya kinidhamu au ya jinai yaliyofanywa na mtumishi yeyote wa Utumishi, Timu ya Majibu ya Haraka imepelekwa katika maeneo ya matukio kukusanya maelekezo," IPOA imesema katika taarifa.
"Hii ni kwa ajili ya kupata habari zote ambazo zinaweza kuwa muhimu katika kufichua mazingira yanayozunguka utekaji nyara na kama kulikuwa na uhusika wa polisi kama inavyodaiwa kwa jumla,” IPOA ilisema.
Mahakama yaongea
Kitengo cha mahakama kimelaani vikali visa vya utekaji nyara ikisema kuna "ripoti za hivi punde za utekaji nyara ulioibuka tena."
"Mahakama imezingatia ripoti za hivi punde za utekaji nyara ulioibuka tena. Kenya ni demokrasia ya kikatiba, ambapo utawala wa sheria unasimama kama thamani ya msingi na kanuni elekezi ya utawala wetu," imesema katika akaunti yake ya X.
"Utekaji nyara hauna nafasi kisheria na kwa hakika ni tishio la moja kwa moja kwa haki za raia. Kwa kuzingatia ripoti hizi, tunahimiza sana mashirika ya usalama na vyombo vyote vilivyounganishwa kuzingatia sheria ili kulinda haki za kimsingi na uhuru.
"Kila anayekiuka sheria lazima akabiliane na nguvu zote za sheria...na kuwateka nyara Wakenya wasio na hatia mitaani ni uhaini na utumiaji wa madaraka ya kinyama...hio si Ukenya !," wakili wa katiba Ahmednasir Abdulahi amesema katika akaunti yake ya X.
viongozi tofauti wataka serikali iwaachilie waliopotea
Aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa visa vya utekaji nyara wa kutatanisha vinavyoendelea nchini.
“Hii ni mbaya na ni kitu cha ajabu sana, hatuwezi kuishi kwenye nchi ambayo watu wanapotea bila sababu nyingine na kuwekwa kimya kwa muda mrefu, lazima serikali ilichukulie kwa uzito jambo hili na kulitatua. wananchi wanataka nchi salama, " Raila alisema Jumatano.
Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki la Mombasa Martin Kivuva pia alielezea wasiwasi sawa na huo, akisema utekaji nyara huo unatishia amani katika Uchaguzi Mkuu ujao wa 2027, akibainisha kuwa sheria inapaswa kuchukua hatua kamili katika kuwakamata wahalifu.
"Utekaji nyara unaofanywa kwa sababu ya kujieleza umepitwa na wakati. Hilo ndilo tuliloshuhudia wakati wa ukoloni ambapo mtu angeteswa kwa kuwa na mawazo tofauti tu," Kivuva alibainisha katika mahubiri yake ya Krismasi.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Kianglikana Kenya Ole Sapit aliwataka wale wanaohusika na utekaji nyara huo wawe wastaarabu na kuacha tabia zao za kihuni.
"Ni ombi letu kwa yeyote aliye nyuma ya hili kuacha na tuchukue hatua kwa uwajibikaji na kuonyesha kwamba tunajali taifa hili na mustakabali wake."
Naye kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo musyoka pia ameongeza sauti yake kwa kulaani utekaji nyara.
"Bwana Ruto, huu ni utawala wa aina gani? Billy Mwangi, Peter Muteti, Naomi na Bernard Kavuli wako wapi? Utekaji nyara huu lazima ukome. Waachilie waliotekwa nyara kwa familia zao mara moja, lazima ukome, " Musyoka alisema akiongea na waandishi wa habari.
Insepkta Jenerali wa Polsii Kenya amesema katika taarifa yake kuwa watu waache kusambaza habari anazoita potofu kuwa polisi inahusika katika utekaji nyara wa wananchi.