Collins Jumaisi ameripotiwa kutoroka kizuizini pamoja na wafungwa wengine  waliokuwa katika Kituo cha Polisi cha Gigiri, Nairobi/ Picha: Wengine 

Maafisa 8 wa polisi nchini Kenya, akiwemo Kamanda wa kituo cha polisi cha Gigiri, Nairobi, wamekamatwa wakilaumiwa kwa kumsaidia Mshukiwa wa mauaji Collins Jumaisi kutoroka na wengine 12.

Hii ni kwa Mujibu wa Kaimu Inspekta mkuu wa Polisi Kenya Gilbert Masengeli.

Mapema Jumanne polisi nchini Kenya ilitangaza kutoroka kwa Collins Jumaisi, ambae ni mshukiwa mkuu wa mauaji ya wanawake ambao miili yao ilipatikana Julai 2024 katika dampo kwenye eneo la Mukuru kwa Njenga, katika eneo la Embakasi, jijini Nairobi.

Ameripotiwa kutoroka kizuizini pamoja na wafungwa wengine 12 waliokuwa katika Kituo cha Polisi cha Gigiri, jijini Nairobi,

Juamisi alishukiwa kwa mauaji ya wanawake 42 kati ya 2022 na 2024.

Kisa cha kutoroka kwake kizuizini kilitokea 20 Agosti 2024, asubuhi.

Kulingana na ripoti ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) huko Gigiri, kutoroka kwao kuligunduliwa mwendo wa saa 11 alfajiri wakati wa ukaguzi wa kawaida.

Vyombo vya habari vya seriklai ya Kenya vinasema miongoni mwa waliotoroka ni pamoja na raia 12 wa Eritrea ambao walikuwa wakishikiliwa kwa ukiukaji wa uhamiaji.

Inaripotiwa polisi waligundua kutoroka kwao wakati wa chai ya asubuhi.

Walikuwa wamekata matundu ya waya ambao ni sehemu ya usalama na kuinua ukuta wa mzunguko.

Mkurugenzi wa DCI Mohamed Amin alithibitisha kisa hicho akisema msako mpya umeanzishwa dhidi ya mshukiwa huyo. "Inasikitisha kuwa hili limetokea lakini tunafuatilia suala hilo kwa hatua," alisema.

Miili katika dampo

Jumaisi alikiri kuwaua hadi wanawake 42 lakini alikanusha mashtaka mbele ya mahakama Julai 2024.

Jumaisi alikuwa amewekwa rumande akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake siku ya Ijumaa.

Miili ya wanawake ilipatikanaJuali 2024 imetupwa katika dampo katika eneo la Mukuru kwa Njenga, katika eneo la Embakasi, jijini Nairobi/ picha: AFP

Polisi Ijumaa iliyopita walipewa siku saba zaidi kuwazuilia washukiwa watatu akiwemo Jumaisi wanaohusishwa na mauaji ya Kware.

Wengine wawili ni Amos Momanyi na Moses Ogembo.

Washukiwa hao walikuwa wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Makadara Irine Gichobi ambapo upande wa mashtaka uliitaka mahakama kuruhusu waendelee kuzuiliwa kwa siku 21.

TRT Afrika