Polisi nchini Kenya wamenasa shehena ya maziwa ya unga yaliyopitiliza muda wake ambayo wanashuku yalilengwa kuuzwa tena dukani.
Oparasheni hiyo iliyoongozwa na kitengo cha polisi cha kukabiliana na uhalifu wa kibiashara iliweza kunasa magunia 1,511 ya maziwa hayo yaliyo haribika yanayo kisiwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola nusu milioni.
Katika taarifa waliochapisha katika mtandao wao wa Twitter, Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi Kenya, DCI, amesema kuwa wameweza kuhusisha shehena hiyo na maziwa yaliyonaswa katika bandari ya Mombasa, ambayo tayari yalikuwa yamegundulika kuwa ni hatari kwa matumizi ya binadamu.
‘Maafisa wetu wameanzisha msako kuwatafuta washukiwa waliopanga uhalifu huo unaohofiwa kuwa na madhara makubwa kwa afya ya binadamu iwapo maziwa hayo yangeingia katika soko,’’ waliongeza.
Polisi hao walifuatilia habari za kudokezewa, walikuta shehena ya magunia ya kilo 25 kila moja ambayo yalikua yametolewa nembo zake na ilani ya tarehe ya mwisho ya kutumiwa.
Maziwa hayo yalichukuliwa kufanyiwa uchunguzi na kutangazwa kuwa yameharibika na ni hatari kwa afya ya binadamu kupitia shirika la kukagua uhalali wa bidhaa Kenya.